Siasa

Gachagua ajutia kumkosea Uhuru heshima

June 1st, 2024 2 min read

WAIKWA MAINA Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais Rigathi Gachagua sasa ameungama waziwazi kwamba yeye na wanasiasa wengine kutoka eneo la Mlima Kenya walikosea kwa kumtusi na kumdhalilisha Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Aliahidi kutorudia kosa hilo la “kumkosea heshima mfalme wetu”.

Akiongea katika eneo la Kimende mnamo Ijumaa akiwa njiani kutoka eneo la Kinangop kaunti ya Nyandarua, Bw Gachagua alitoa wito kwa viongozi wa Mlima Kenya kuungana ndiposa wawe na nguvu ya kutetea masilahi ya wakazi na wenyeji katika serikali ya Kenya Kwanza.

“Liwe liwalo, kamwe hatutamshambulia tena mfalme wetu. Tulizunguka hapa tukimtukana na kumkosea heshima. Niliomba msamaha kwa kosa hilo. Si mtanisamehe. Hatutarudia kosa hili la kumtusi mfalme wa jamii ya Agikuyu. Tuwafunze vijana wetu kwamba wasithubutu kutumiwa na watu wengine kumtusi kiongozi wetu. Tupendane ili tupate mgao wetu kwa keki ya kitaifa,” Bw Gachagua akaambia umati wa watu katika eneo la Kimende, Kaunti ya Kiambu.

Naibu Rais Rigathi Gachagua. PICHA | MAKTABA

Kabla na miezi michache baada ya uchaguzi mkuu wa 2022, Bw Gachagua aliwaongoza wanasiasa kutoka Mlima Kenya kumshambulia Bw Kenyatta, mamake Mama Ngina Kenyatta na familia nzima ya Hayati Mzee Jomo Kenyatta.

Mapema mwaka 2023, Bw Gachagua aliitaka familia hiyo kurejesha kwa wajukuu wa Maumau mapande ya ardhi aliyodai walinyakuwa kutoka kwao wakati wa utawala wa Rais wa Kwanza nchini – Hayati Kenyatta.

Ni baada ya kauli kama hiyo kutolewa na Bw Gachagua na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah ambapo wahuni walivamia shamba la familia ya Kenyatta la Northlands katika eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

Wahuni hao waliharibu miti na kuiba zaidi ya mbuzi na kondoo 100 katika shamba hilo la ukubwa wa ekari 100.

Ni baada ya tukio la Machi 29, 2023, ambapo mnamo Julai 4, 2023, Mama Ngina alipokonywa walinzi katika makazi yake ya Muthaiga na Ichaweri, Gatundu Kusini, kaunti ya Kiambu, pasina serikali kutoa sababu zozote maalum.

Lakini mnamo Aprili 2024 akiwa katika eneo la Njabini, Nyandarua, kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa msemaji wa polisi King’ori Mwangi, Bw Gachagua aliomba msamaha kwa Mama Ngina Kenyatta na familia yake kwa “dhuluma ambazo huenda yeye pamoja na viongozi fulani wa Mlima Kenya huenda waliwatendea”.

Bw Kenyatta aliunga mkono kiongozi wa upinzani Raila Odinga katika uchaguzi wa urais dhidi ya Rais William Ruto.

Wiki jana, Bw Gachagua alilamika kuwa kuna wanasiasa fulani kutoka Rift Valley, walioko karibu na bosi wake Dkt Ruto, ambao huzuru eneo la Mlima Kenya kuendesha kampeni za kumjumu kisiasa.

Aidha, aliwakaripia vikali wanasiasa kutoka eneo hilo la Mlima Kenya aliodai “kuungana na watu kutoka sehemu zingine kunihujumu na kupanda mbegu ya migawanyika katika jamii ya Gema.”