Michezo

Gachagua akamilisha mbio za mita 100 licha ya kujikwaa

January 9th, 2024 1 min read

Na MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua kwa sasa anajivunia kasi ya sekunde 59.8 katika mbio za mita 100 baada ya kujizatiti kadri ya uwezo wake mnamo Jumapili.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza ambapo Naibu Rais alitimka mbio huku akihesabiwa muda kama ilivyofanyika katika mashindano ya mbio za nyika za Tinderet katika Kaunti ya Nandi.

Wandani wake walisema muda huo ungekuwa bora zaidi lakini Bw Gachagua alijikwaa akiwa amebakisha hatua chache tu afike utepeni.

Muda bora zaidi kwa Mkenya katika mbio hizo ni wa sekunde 9.77 ambao umewekwa na Ferdinand Omanyala huku rekodi ya Ulimwengu ikiwa ni ya sekunde 9.58 yake mwanariadha Usain Bolt. Kwa wanawake, rekodi hiyo ulimwenguni inashikiliwa na Florence Griffith ya sekunde 10.49.

Mbio hizo katika Kaunti ya Nandi zilikuwa za muigo kati yake na Mkuu wa Utumishi wa Umma Bw Felix Koskei ambaye aliibuka wa pili, wengine wakifuata bila mpangilio wowote.

Bw Gachagua alikuwa amefika katika kaunti hiyo kwa ziara ya kikazi na ambapo alifika kushuhudia mbio hizo za kusaka talanta eneo hilo. Zilivutia maelfu ya wanariadha.

“Naibu Rais Bw Gachagua alijitahidi licha ya kujikwaa na akakamilisha mbio hizo akiwa wa kwanza,” akasema afisa mmoja wa usalama aliyekuwa katika uwanja huo.

Wengine katika mbio hizo walikuwa ni Gavana wa Nandi Bw Stephen Sang, Naibu Gavana wa Nandi Bw Yulita Mitei, Rais wa Athletics Kenya Bw Jackson Tuwei na Katibu katika wizara ya Michezo Peter Tum.

Wabunge walikuwa Julius Melly wa Tinderet, Zipporah Kering’ wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Joseph Cherorot wa Kipkelion Mashariki, Hillary Kosgey wa Kipkelion Magharibi, Marianne Kitany (Aldai), Paul Biego (Chesumei), mwenzao wa Mosop Bw Ibrahim Kirwa, Josses Lelmengit wa Emgwen, na Bernard Kitur wa Nandi Hills.