Habari Mseto

Gachagua amtembelea hospitalini polisi aliyedungwa mishale na washukiwa wa upishi wa chang’aa

April 2nd, 2024 1 min read

Na MWANGI MUIRURI

NAIBU wa Rais Rigathi Gachagua mnamo Aprili 2, 2024 alimtembelea Kamanda wa polisi wa kituo cha Juja Bw John Misoi ambaye amelazwa hospitalini baada ya kupigwa mishale na wapishi wa chang’aa mnamo Jumapili usiku. 

Bw Gachagua aliahidi afisa huyo usaidizi wa serikali na pia akaahidi kwamba waliotekeleza shambulizi hilo lililofanyika katika mtaa wa Gachororo watakamatwa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Kiambu Bw Michael Muchiri, afisa huyo alikuwa ameandamana na maafisa wake katika eneo moja la maandalizi ya pombe haramu na pia mihadarati.

“Maafisa hao walikuwa wamedokezewa kulikuwa na biashara ya pombe haramu na mihadarati. Afisa huyo aliongoza kikosi chake na wakavamia maskani hiyo,” akasema.

Bw Muchiri alisema kwamba usalama katika danguro hilo ulikuwa umewekwa na wahuni waliokuwa wamejihami kwa vifaa butu na walioishia kumpiga mishale Chifu Inspekta Misoi.

Soma pia OCS wa Juja adungwa mishale na wapishi wa chang’aa