Habari za Kitaifa

Gachagua amwomba msamaha Mama Ngina Kenyatta

March 25th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

NAIBU Rais Rigathi Gachagua mnamo Jumatatu Machi 25, 2024 alimwomba msamaha mamake Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, Mama Ngina Kenyatta, kutokana na matamshi makali yaliyoelekezwa kwake na wanasiasa wa Kenya Kwanza wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Gachagua alitaja matamshi hayo kama ya kusikitisha, akisema kuwa “ni jambo ambalo hangependa lijirudie tena”.

Kwenye mahojiano na kituo cha redio cha Kameme FM, Bw Gachagua alisema anamtambua Mama Ngina kama mzazi na mwanamke wa hadhi anayeheshimika katika ukanda wa Mlima Kenya na nchini kote kwa jumla.

“Kwa kweli, singependa turejee tulikokuwa. Nasikitika sana kwamba tulitoa matamshi mabaya dhidi ya Mama Ngina, licha ya kuwa mzazi na mwanamke anayeheshimika. Hata kama ulikuwa ushindani wa kisiasa, tulivuka mipaka. Kwa hivyo, ninamwomba msamaha, na ninamrai atusamehe. Ninawaahidi wakazi wote wa Mlima Kenya kwamba jambo hilo halitajirudia tena. Hata ikiwa ni siasa, afadhali nisikuwepo,” akasema Bw Gachagua.

Kulingana na wadadisi wa siasa, lengo kuu la Bw Gachagua ni kujisawiri kama kiongozi muungwana, asiye na tofauti yoyote ya kisiasa na eneo lolote katika ukanda wa Mlima Kenya.

Wanasema kuwa kwa kuomba msamaha huo, lengo la Bw Gachagua ni kutafuta mpenyo wa kisiasa katika Kaunti ya Kiambu, ikizingatiwa kuwa Mama Ngina ni mkazi wa kaunti hiyo.

“Ukweli ni kuwa, ombi la msamaha la Bw Gachagua kwa Mama Ngina linalenga kumsaidia kupenya kisiasa katika Kaunti ya Kiambu, ikizingatiwa kuwa kuna watu waliohisi kukosewa na matamshi makali ya Naibu Rais na washirika wake katika Kenya Kwanza dhidi yake (Mama Ngina).

“Ni hatua nzuri ya kukabili upinzani wa kisiasa ambao amekuwa akikabiliwa nao, kwa mfano kutoka kwa Waziri wa Utumishi wa Umma, Moses Kuria, ambaye ni mkazi wa Kiambu,” asema Bw Micah Mutai, ambaye ni mdadisi wa masuala ya kisiasa.

Hapo awali, viongozi kadhaa wa Chama cha Jubilee (JP) walikuwa wamemshinikiza Bw Gachagua kumwomba msamaha Bw Kenyatta na Mama Ngina kutokana na matamshi hayo na uvamizi uliotekelezwa na watu wasiojulikana dhidi ya shamba la Northlands, Ruiru, linalomilikiwa na familia ya Kenyatta.

Baadhi ya viongozi waliotoa masharti hayo ni Katibu Mkuu wa JP, Bw Jeremiah Kioni.