Habari Mseto

Gachagua aonya wakeketaji wa wasichana Samburu

June 7th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua ameonya mitandao ya kuvumisha ukeketaji wa wasichana katika Kaunti ya Samburu kwamba itaangamizwa kwa vyovyote vile.

Aliwataka watu wenye kuendeleza mila hiyo kukoma mara moja.

“Msitujaribu kamwe. Mimi sitaki kusikia mambo kama hayo ya kipuzi na ambayo yamepitwa na wakati. Ukeketaji wa wasichana ni mila ambayo imepitwa na wakati na inakiuka hata maadili ya utu. Ni mila ambayo hata haifai kuwa ikirejelewa katika mijadala yoyote,” akasema Bw Gachagua.

Alisema kwamba hata akiwa Nairobi, atakuwa akifuatilia kwa karibu matukio katika Kaunti ya Samburu.

“Lengo ni kuhakikisha hawa wasichana wetu wadogo wanapata nafasi ya kusoma na kuwa katika usalama wa kila aina ndio waafikie kiwango cha juu cha uwezo wao katika jamii,” akasema.

Bw Gachagua alikuwa akiongea katika shule ya upili ya kitaifa ya Kisima ambapo alitoa mchango wa Sh5 milioni, pesa ambazo zitatumika kujenga bweni la wanafunzi.

“Hawa wasichana wakiangaliwa vyema na wapigwe jeki kikamilifu, watakuwa ndio kesho yetu katika kupata hata viongozi wa kuendesha masuala ya kaunti na pia taifa kwa ujumla,” akasema.

Aidha, aliwataka maafisa wa usalama katika kaunti hiyo kukabiliana na ujangili hasa ule wa wizi wa mifugo.

“Nimefurahia kuona kwamba visa vya ujangili wa wizi wa mifugo vimedhibitiwa kwa kiwango kikuu kupitia kazi ya bidii ya maafisa wetu wa usalama. Tieni bidii ili kaunti hii iwe na amani wa kuwezesha wenyeji kushiriki kiikamilifu harakati za kimaendeleo. Hao wezi ni lazima wapambanwe nao ndio tuwe na amani na maendeleo hapa Samburu,” akasema.

Alimtaka mbunge wa Samburu Magharibi Bi Naisula Lesuuda aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha Kanu, ahamie mrengo wa Kenya Kwanza Alliance (KKA) akisema “wewe ni mtu mzuri na hufai kukaa huko nje ukigugunwa na baridi”.

Bw Gachagua alisema kwamba “uchaguzi uliisha na sote tunafaa tuungane kuwafanyia wakenya kazi pasipo kuzingatia mirengo ya vyama”.

Alisema kwamba “nitafurahia sana kukuona katika timu yetu tukitafutia Rais William Ruto kura za awamu ya pili 2027 kwa kuwa ninakutambua kwamba wewe ni mchezaji mzuri wa siasa”.