Habari Mseto

Gachagua apondwa na wabunge kwa kutumia ndege ya KQ kwenda Mombasa

June 13th, 2024 3 min read

NA CHARLES WASONGA

SIKU moja baada ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kutumia ndege ya abiria ya shirika la Kenya Airways (KQ) kwa safari ya kutoka Nairobi kwenda Mombasa, wabunge wamemponda vikali.

Wakiongozwa na kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wah na mwenza wa mrengo wa wachache Opiyo Wandayi, wabunge wa mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio walidai kitendo hicho kinashusha hadhi ya Afisi ya Naibu Rais.

“Bunge hili huzitengea afisi ya Naibu Rais, afisi ya Rais na ile ya Mkuu wa Mawaziri mamilioni ya fedha kila mwaka za usafiri nchini na nje. Japo sio vibaya kwa naibu rais kutumia ndege ya KQ, mbona alijianika katika uwanja wa ndege wa JKIA akiburuta mkoba kana kwamba hana wasaidizi wa kumbebea mizigo yake anaposafiri? Hii ni aibu kubwa kwa afisa ya hadhi kama ya Naibu Rais,” akasema Bw Ichung’wah ambaye ni Mbunge wa Kikuyu.

“Alilenga kutimiza lengo gani kwa kuagiza wapiga picha katika afisi yake kumpiga picha akijikokota na mkoba akiabiri ndege kisha akawaagiza wasambaze picha hizo mitandaoni?” akauliza tena Jumatano wakati wa kikao cha alasiri.

Bw Ichung’wah alimtaka Bw Gachagua kukoma kushiriki sarakasi zisizo na maana akinuia kuonyesha kuwa anadhulumiwa na serikali kwa kuzimwa kukodisha ndege kusafiria inavyopasa kulingana na taratibu serikali.

Kwa upande wake, Bw Wandayi alimwonya Bw Gachagua dhidi ya kuibua mzaha na hivyo kushusha hadhi ya Afisi hiyo ya pili kwa mamlaka nchini Kenya.

“Ikiwa Bw Gachagua aliongozwa na lengo la kupunguza matumizi ya pesa za serikali mbona aliandamana na ujumbe mkubwa katika safari yake ya kwenda Mombasa. Mbona akaandamana na zaidi ya walinzi 14 na hata wanablogu akiwemo Mbunge wa zamani wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu?” akauliza Bw Wandayi, ambaye pia ni Mbunge wa Ugunja (ODM).

Kiongozi huyo wa wachache katika Bunge la Kitaifa vilevile aliwataka Rais William Ruto, Bw Gachagua na wabunge wa mrengo wa Kenya Kwanza kukomesha malumbano ya kila mara akisema wanatoa taaswira kwamba wameshindwa kuongoza nchini.

Wengine waliomsuta Bw Gachagua kwa kuabiri ndege ya abiria ya KQ ni Kiranja wa Wengi Sylvanus Osoro, Kiranja wa Wachache Junet Mohamed na wabunge Didmus Barasa (Kimilili), T. J Kajwang’ (Ruaraka), John Mukunji (Manyatta) Dancan Mathenge (Nyeri Mjini) na Mbunge Mwakilishi wa Mombasa Bi Mohammed Zamzam.

“Ilikuwa aibu kwa Naibu Rais akionekana katika uwanja wa ndege akizunguka huku na huku akibeba mkoba kama kile kilichoonekana kama kitendo cha uhusiano mwema. Wafanyakazi katika afisi yake walikuwa wapi? Na mbona wahudumu wa shirika la KQ au mamlaka ya usimamizi wa viwanja vya ndege angalau hawakumsaidia kuubeba mkoba huo?” Bw Osoro akauliza.

Bw Junet alizuia kicheko alipopendekeza kuwa bunge la kitaifa libuni kamati maalum la kuchunguza kile ambacho Bw Gachagua alikuwa amebeba katika mkoba huo.

“Kwa sababu huyo jamaa anashikilia afisi ya umma, na sio kawaida kwa afisa wa serikali wa hadhi yake kujibebea mkoba au mzigo wowote anaposafiri, sisi kama wabunge na wawakilishi wa Wakenya twapaswa kuchunguza kubaini kile ambacho alikibeba ndani ya mkoba ule,” akasema huku wabunge wenzake wakiangua kicheko.

Mnamo Jumanne, Juni 11, 2024 Wakenya wa matabaka mbalimbali waliachwa vinywa wazi picha zilipomwonyesha Bw Gachagua akiabiri ndege ya KQ akiubeba mkoba wake mwenyewe.

Bw Gachagua alionekana akiwasili katika uwanja wa JKIA, Naiobi akiwa amebeba mkoba wake tayari kuabiri ndege ya KQ kama abiria wa kawaida.

Katika picha nyingine alionekana akiingia ndani ya ndege akiwa anaburura mkoba huo akielekezwa na wahudumu wa shirika la KQ.

Duru za afisi ya Naibu Rais ziliambia Taifa Leo kwamba Bw Gachagua alikuwa akielekea Mombasa kuongoza ufunguzi rasmi wa Kongamano la Kisayansi la Kimataifa la Chama cha Wanafamasia wa Kenya.

Shughuli hiyo ilifanyika Jumatano Juni 12, 2024 katika mkahawa wa Sarova Whitesands, mjini Mombasa.

Katika siku za hivi karibuni, wandani wa Bw Gachagua wakiongozwa na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga wamekuwa wakilalamikia kile wanachokitaja kama kudhalilishwa kwa Bw Gachagua kwa kunyimwa nafasi ya kutumia ndege za kijeshi.

Jumapili, Gachagua pia alionyesha hali hiyo alipodai kuwasili kuchelewa katika kongamano la Dhehebu la Akorino mjini Nakuru kutokana na kile alichokitaja kama “changamoto ya usafiri”

Majuma mawili yaliyopita Waziri wa Ulinzi Aden Duale alipiga marufuku wanasiasa, isipokuwa Rais, kutumia helikopta na vyombo vingine vya usafiri vya jeshi la ulinzi la Kenya (KDF).

Jumatano, Juni 12, 2024 Bw Ichung’wah aliwaambia wabunge kwamba ilivyo sasa ni Rais Ruto pekee ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu anayeruhusiwa kutumia ndege za KDF katika safari zake nchini.

“Naibu Rais ametengewa helikopta ya polisi ambayo wakati huu inafanyiwa ukarabati. Hata hivyo, akiwasilisha ombi la kutumia ndege za KDF na akubaliwe, sharti afisi yake igharamie mafuta,” Bw Ichung’wah akafafanua.