Siasa

Niko na Ruto, anayetaka kunisuta aje Mlimani – Gachagua

June 6th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua sasa anawataka wanasiasa wote wa Mlima Kenya walio na dhana kwamba wako na ubabe wa kisiasa kumliko katika eneo hilo, wafanye hima kuthubutu kuandaa mkutano wa ajenda hiyo katika mipaka ya eneo hilo.

Bw Gachagua alisema ni kupitia njia hiyo ambapo watakumbana na sura yake kamili ya kisiasa “badala ya kunipiga mkiwa mbali na kwetu mkitumia usaidizi wa wengine wasio wetu na majukwaa yaliyopangwa na wengine”.

“Ikiwa wewe ni mwanamume wa kweli, jaribu tu kuuleta huo mkutano wa kupigana nami na kupinga kile ambacho ni kutetea masilahi ya Mlima Kenya katika mipaka yetu. Hapo ndipo tutakutambua kwamba unajielewa na ndipo utakumbana nasi walio wengi eneo hili,” akasema Bw Gachagua mnamo Jumatano katika eneobunge la Mukurwe-ini lililoko Kaunti ya Nyeri.

Eneobunge la Mukurwe-ini hupakana na lile la Kiharu ambalo huwakilishwa na Bw Ndindi Nyoro.

Naibu Rais amekuwa akionekana kuwa ndani ya msukosuko wa kisiasa ambao unasemwa kutokana na hotuba za baadhi ya wanasiasa wakiwemo mshauri mkuu wa Rais William Ruto kuhusu uchumi Dkt David Ndii, Bw Nyoro, Waziri wa Utumishi wa Umma Bw Moses Kuria, Gavana wa Kirinayaga Bi Anne Waiguru na mbunge wa Laikipia Mashariki Bw Mwangi Kiunjuri.

Ajabu ya siasa za sasa eneo hilo ni kwamba, Bw Gachagua anasikika akiongea lugha moja na wanasiasa wa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya ambao wanasisistiza umoja wa wenyeji wa Mlima Kenya na masilahi yao yachungwe kikamilifu na utawala wa serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Dkt Ruto.

Washirika hao wa Azimio eneo la Mlima Kenya wameunda muungano wao wanaouita Haki, wakisema watautumia kuitimua serikali ya sasa mamlakani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Pale wakereketwa wa Azimio hawajaafikiana na Bw Gachagua ni kuhusu ufaafu wa Rais Ruto kupata awamu ya pili katika uchaguzi wa 2027, wakisema ang’olewe naye naye Bw Gachagua akisema anafaa kutawala miaka 10 bila breki.

Naibu Rais alieleza kwamba wito wake kwamba watu wa Mlima Kenya waungane unalenga pia kuwaambia wamuunge yeye pamoja na Dkt Ruto kwa manufaa yao na Wakenya kwa ujumla.

“Walio na usaliti kwa masilahi yetu wako na mtindo wa kusema maneno yao wakiwa katika mikutano ya kisiasa iliyoandaliwa katika maeneo yaliyo nje ya hapa kwetu,” akasema Bw Gachagua.

Alisema pia vita hivyo vya kuuvuruga umoja wa Mlima Kenya vinaendelezwa katika mitandao ya kijamii inayodhibitiwa au kuendeshwa wa wengine kutoka nje ya mipaka hiyo ya kwao.

“Mimi ninakutangazia wazi kwamba ikiwa unajielewa, kuja hapa kwetu na uandae mkutano wa kisiasa wa kusema tusiungane, kahawa yetu isilipwe bei nzuri na tusifutiwe madeni. Useme mgao wa rasilimali kwa msingi wa idadi ya watu sio wazo la busara na pia useme sisi watu wa Mlima Kenya hatufai kuongea kwa sauti moja,” akasema, akiongeza kwamba hakuna mjadala wa ni nani mkuu wa siasa za eneo hilo “kwa kuwa ni mimi”.

Bw Gachagua alishikilia kwamba yeyote aliye na mawazo ya kuhujumu umoja wa eneo hilo akiwa mwenyeji ataandaliwa mikakati thabiti ya kisiasa kwa nia ya kummaliza.

Naibu huyo wa rais alisema kwamba “ule wakati wa kunyonyeshana kidevu umeisha na ni lazima kwa sasa tushikane ili tuvukishe eneo hili hadi kwa yale manufaa yanayohitajika kabla ya 2027 kufika”.