Makala

Gachagua: Awali, watoto wangu hawakuunga azma ya Ruto kuwa Rais


NAIBU Rais Rigathi Gachagua amefichua kuwa watoto wake hawakuunga mkono azma ya Rais William Ruto kuwa kiongozi wa taifa la Kenya.

Kulingana na Bw Gachagua, suala hili lilikuwa zito kiasi cha kugawanya familia katikati alipowaambia wapige kura kama familia.

Bw Gachagua na mkewe, Pasta Dorcas Gachagua walikuwa upande mmoja, ilhali wanawe wawili walikuwa wakipinga Dkt Ruto kuchaguliwa kama Rais wa Jamhuri ya Kenya.

Naibu Rais alifichua haya katika ibada kanisani Kaplong Deliverance Sotik, Kaunti ya Bomet mnamo Jumapili, Juni 30.

Kwa mujibu wa masimulizi yake, ilibidi aongoze familia kuwa na sauti moja.

Kulingana na Naibu Rais, hapo ndipo wana wake walimuunga mkono Dkt Ruto.

Licha ya watoto wake, ambao ni; Keith na Kevin, kuhofia kupinga utawala uliopita, Bw Gachagua alisema kuwa aliamini kuwa Dkt Ruto alikuwa mgombeaji wa urais aliyefaa.

“Wakati mwingine tulikosana hadi mama yao ilibidi aingilie kati. Wacha niwaambie, zile siku tulimuunga mkono Rais William Ruto, tulikumbana na matatizo mengi sana kwa sababu tulikuwa tunaenda kinyume na maelekezo ya serikali,” alisema.

Aliendelea kusimulia kuwa jinsi utawala uliopita ulimwomba akome kumuunga mkono Dkt Ruto ambaye wakati huo alikuwa Naibu Rais.

Ruto alihudumu kama naibu rais kati ya 2013 na 2022.

Bw Gachagua alisema uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta ulifika viwango vya kutisha kumtupa jela, akiaandamwa na kesi nyingi kortini.

“Hata hivyo, ilibidi nikae na Rais Ruto kwa sababu niliamini alipokuwa anatupeleka. Mke wangu, Mchungaji Dorcas, aliniunga mkono. Tulikuwa wawili dhidi ya wawili.  Na kama mwenyekiti wa mkutano, nilipiga kura ya mwisho na sote tukaelewana kumpigia kura Dkt Ruto,” alisema.

Haya yanajiri huku mpasuko katika chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA), kinachoongozwa na Rais Ruto, ukizidi kukithiri.

Bw Gachagua hata hivyo alisema suala la kudorora kwa uhusiano kati yake na Rais linashughulikiwa katika msingi wa maendeleo, umoja na demokrasia.

Vile vile, alidokeza mzozo unaotikisa Muungano wa Kenya Kwanza unachochewa na viongozi waliojiunga na serikali.