Gachagua, Karua wapiga kura Sagana na Mugumo mtawalia

Gachagua, Karua wapiga kura Sagana na Mugumo mtawalia

GEORGE MUNENE Na STEPHEN MUNYIRI

MGOMBEA mwenza wa Raila Odinga katika muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Martha Karua Jumanne amesifu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka kwa kuendesha shughuli ya upigaji kura kwa njia inayofaa.

Ingawa hivyo, amesikitika kwamba utaratibu wenyewe ulikuwa ni wa mwendo wa kobe.

Mwanzo alipofika katika kituo cha Shule ya Msingi ya Mugumo katika Kaunti ya Kirinyaga, mbunge huyo wa zamani wa Gichugu aliangaliwa ikiwa jina lake liko kwa rejista ya IEBC. Lilikosekana katika chumba cha kwanza akaelekezwa katika chumba cha pili ambako maafisa wa uchaguzi walipata jina lake kwenye sajili ya wapigakura hivyo akapiga kura.

“Japo shughuli hii inaenda polepole, kila kitu kiko sawa. Kwa mfano nilipoingia katika chumba cha kwanza katika kituo hiki jina langu lilikosekana. Nilielekezwa hadi kwa chumba cha pili ambapo jina langu lilipatikana katika sajili ya wapigakura,” amesema.

Amepiga kura saa kumi na mbili na nusu asubuhi.

“Tangu nijitose kwa siasa nina mazoea ya kupiga kura asubuhi na mapema,” amesema akiwarai wapigakura wajitokeze kwa wingi waamue mustakabali wa Kenya.

Alifika kituoni akiwa na wazazi wake na wanafamilia wengine.

Kwingineko katika eneobunge la Mathira, mgombea mwenza wa Dkt William Ruto katika chama cha United Democratic Alliance (UDA) ndani ya muungano wa Kenya Kwanza Rigathi Gachagua  amewasili katika kituo cha Shule ya Msingi ya Sagana, Kaunti ya Nyeri saa moja asubuhi akiwa na mkewe Dorcas Rigathi pamoja na shangazi yake Bi Gladys Karaba. Watatu hao walifika katika kituo hicho saa moja asubuhi kupiga kura. Shangazi yake Rigathi anaishi na ulemavu na amesaidiwa kupiga kura.

“Nimefurahi kuona wapigakura wakianza kutoka katika makazi yao saa tisa asubuhi katika eneo letu la Mlima Kenya ili wapate fursa ya kuwachagua viongozi wao,” amesema Gachagua.

Katika maeneo mbalimbali kaunti za Kirinyaga na Nyeri, wakazi wamevumilia baridi kali na hata manyunyu hapa na pale.

  • Tags

You can share this post!

Kipchoge afungua maktaba kwa umma Kapsisiywa

Hakuna kura ya ugavana Mombasa, Kakamega leo

T L