Jamvi La Siasa

Gachagua lawamani kwa kujiuma ulimi akiwa Nyeri

May 4th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

KAULI aliyotoa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwamba anatumia mamlaka yake afisini kusaidia Nyeri kujipa minofu ya serikali, imeibua minong’ono.

Wadau katika ukanda wa Mlima Kenya wamegawanyika, baadhi wakiikemea huku wengine wakidai kauli ya Bw Gachagua ni majazi ya kujumuisha ngome yote ya Mlimani.

“Sisi tuliambiwa kwamba serikali ni yetu hapa Mlima Kenya ambapo tuko na kaunti 11. Kura zilipeanwa kwa serikali iliyoko mamlakani kwa kiwango cha asilimia 87 hapa Mlima Kenya upinzani ukijizolea asilimia 13 pekee. Lakini kwa sasa Bw Gachagua amekiri waziwazi kwamba anatumia nafasi yake kuifaa ngome yake ya Nyeri,” akasema mshirikishi wa vuguvugu la vijana wanataaluma wa Mlima Menya, Bw Moses Warui.

Akiongea katika mazishi ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la AIPCA mnamo Aprili 30, 2024, katika kijiji cha Ihithe kilichoko Kaunti ya Nyeri, Bw Gachagua alisimulia kwa Lugha ya Gikuyu ambapo alisifu umoja wa viongozi wa Kaunti ya Nyeri.

“Huu umoja wa viongozi wa watu wa Nyeri umenipa hadhi kuu katika serikali ya Rais William Ruto kwa kuwa ameniaminia majukumu ya kuzima mizozo katika kaunti zilizoko ndani ya ngome zetu za kisiasa. Wakati kwangu nyumbani kuna amani, ninapewa heshima hata ya kutatua mizozo kwingineko,” akasema Bw Gachagua.

Ni huo umoja na amani katika Kaunti ya Nyeri ambapo Bw Gachagua alikiri kwamba vimesaidia eneo hilo kujipa minofu ya migao ya serikali.

“Hayo tumepata kama watu wa Nyeri hayatoshi… mengine mengi yaja. Kuna kitu ninapanga hivi karibuni. Mimi nikisikia nafasi ikitokea, nakuwa macho na nimetega masikio. Hatimaye huwa ninawaita hawa viongozi wa Nyeri na tunaulizana ni wapi hatujagawa keki…Tukielewana tunazawadi,” akasema.

Waombolezaji watoa heshima za mwisho kwenye mazishi ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la AIPCA mnamo Aprili 30, 2024, katika kijiji cha Ihithe kilichoko Kaunti ya Nyeri. PICHA | MWANGI MUIRURI

Kwa sasa, Kaunti ya Nyeri inajivunia mgao wa hivi majuzi ambapo Mkuu wa Majeshi (CDF) Jenerali Charles Muriu Kahariri aliyeapishwa Ijumaa na Rais William Ruto kuchukua mahali pa marehemu Francis Ogolla, ni mzawa wa eneobunge la Kieni.

Jenerali Ogolla aliaga dunia katika mkasa wa ajali ya ndege mnamo Aprili 18, 2024, akiwa katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Katika hotuba yake inayozua utata, Bw Gachagua alisema kwamba “huwa inalilia ile yake inayoihusu”, ukiwa ni msemo wa jamii ya Agikuyu unaomaanisha mama (awe ni wa binadamu au mnyama) hulilia mtoto wake.

Alisema kwamba Kaunti ya Nyeri ni lazima ipate mgao unaoifaa na unaolingana na kura ambazo wenyeji walipigia Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Ni matamshi ambayo yamekera baadhi ya viongozi wa Kaunti nyingine, mwenyekiti wa chama cha Jubilee katika Kaunti ya Kirinyaga Bw Muriithi Kang’ara akimkumbusha Bw Gachagua kwamba Mlima Kenya uko na kaunti nyingi ambazo ziliwinda serikali iliyoko kwa pamoja.

“Tuko na Murang’a, Kirinyaga, Nyeri, Laikipia, Meru, Tharaka Nithi, Embu, Nyandarua, Nairobi, Kiambu na Nakuru… Kusema Kaunti ya Nyeri ndio inazingatiwa kwa kiwango kikuu katika migao ya minofu ni hujuma kuu na kauli hatari kisiasa,” akasema Bw Kang’ara.

Aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi alisema kwamba “ingekuwa ni mimi niliyekuwa na kipaza sauti hicho cha Bw Gachagua, ningeamua kunyamaza kuhusu suala hilo. Lakini sasa kwa sababu alinena hayo, ni shida yake mwenyewe kuhusu athari husika”.

Bw Ngugi alisema “kuna mambo ya siri na ya ndani ambayo hata uking’atwa kwa meno katika kitovu, unanyamaza na usiseme kitu”.

“Suala kama hilo la kuashiria ubinafsi ni mojawapo ya hayo ya kunyamazia,” akasema Bw Ngugi.

Aliyekuwa mbunge wa Ndaragwa Bw Jeremiah Kioni aliteta kwamba “hotuba hiyo ilikuwa kejeli kwa kaunti zote 10 za Mlima Kenya ila tu ya Nyeri… hali ya ubinafsi ambayo kinara wetu wa siasa za Mlima Kenya, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, hajawahi kutekeleza”.

Seneta wa Murang’a Joe Nyutu alisema kwamba “ndio sababu tunasema kuna haja ya kuwa na kiongozi ambaye ni wa kuunganisha Mlima Kenya kwa usawa na kwa haki na niliye naye kwa mawazo yangu sio mwingine bali ni Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro”.

Mwenyekiti wa Baraza la Agikuyu Wachira Kiago aliteta kwamba “wakati tunatarajia Mlima Kenya tuungane na tuongee kwa sauti moja, kunazuka hali ya kuhujumu ari hiyo kupitia matamshi ya kutenganisha watu kwa msingi wa maendeleo”.

Bw Kiago alisema hali hiyo itamtatiza Bw Gachagua si haba katika siasa za Mlima Kenya.

“Ule mgawanyiko wa kimaeneo ambao tunazidi kukataa ujitokeze ndio huo ulipaliliwa kunawiri kupitia matamshi hayo ya mapendeleo,” akasema Bw Kiago.