Habari Mseto

Gachagua: Mniombee niendelee kuwa mkweli


NAIBU Rais Rigathi Gachagua ameihimiza jamii ya Kikristu kumuombea ili aendelee kuwa mkweli katika jitihada zake kuhudumia taifa na pia kusaidia Rais William Ruto kutekeleza ahadi zake kwa Wakenya.

Bw Gachagua, ambaye katika siku za hivi karibuni ameonekana kupambana na mawimbi ya ndani kwa ndani katika chama tawala cha UDA anachosisitiza alisaidia kupata mamlaka, alisema ni kwa maombi pekee yeye na kiongozi wa nchi watafanikiwa kuafikia waliyoahidi Wakenya.

Akizungumza Jumapili, Juni 16, 2024 aliposhiriki ibada ya misa katika kanisa la PMCA, Kaunti ya Kericho, Bw Gachagua aliambia waumini kuombea Rais Ruto apate hekima na ujasiri kuongoza nchi na kuboresha uchumi.

“Mnikumbuke kwenye maombi ili niendelee kuwa mkweli,” Bw Gachagua akasema.

Naibu Rais aliongoza kanisa la PMCA, Kericho kufanya mchango.

Matamshi ya Gachagua yamejiri wiki chache baada ya mzozo ambao umekuwa ukiendelea kutokota kati yake na wanachama wa UDA kuhusu msimamo wake kama msaidizi wa Dkt Ruto serikalini, kuonekana kuibuka hadharani.

Wanasiasa wa UDA, wandani wa Rais Ruto, wamekuwa wakimshambulia Gachagua kimaneno, hatua inayoonekana kutomridhisha mbunge huyo wa zamani Mathira.

Aidha, amekuwa akilalamikia kuhujumiwa katika serikali aliyosaidia kuunda 2022.

Kuchelewa kwake mara kwa mara katika hafla za Kitaifa na kisa cha majuzi kuabiri ndege ya KQ kuelekea Mombasa, ni kati ya malalamishi aliyoibua Bw Gachagua akidai kunyimwa raslimali za serikali kuhudumu.

Kwa sababu hii, inasemekana kuna uwezekano amehamia kambi ya upinzani inayoongozwa na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga baada ya Bw Raila na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, kuunga mkono mfumo wake wa ugavi wa raslimali wa ‘Shilingi moja, kura moja, mtu mmoja”.

Kampeni hiyo amekuwa akiivumisha ngome yake ya Mlima Kenya.

Licha ya mpasuko kuonekana kujiri kati yake na Rais Ruto, Gachagua ameshikilia msimamo wake kuwa hajamuacha kiongozi wa nchi.

Naye Rais Ruto anaonekana kushikilia msimamo huo huo kwani amewakataza hadharani wanachama wa UDA kumsuta naibu wake kwa maamuzi yake.

Akiwa Kericho, Bw Gachagua aliwataka wanahabari waandike habari sisizoegemea upande mmoja wa kisiasa.