Habari za Kitaifa

Gachagua: Ruto alikuwa anafurahi sana nilipokuwa natusi familia ya Kenyatta


MATAMASHI makali aliyoyatoa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuhusu masaibu yake serikalini yameanika wazi mikwaruzano ya kisiasa ambayo imekuwa ikiendelea kati yake na mrengo wa Rais William Ruto katika serikali ya Kenya Kwanza.

Akizungumza na vituo vya habari mnamo Jumapili, Bw Gachagua alilaumu serikali kwa kuwahangaisha wandani wake, akagusia hoja ambayo imekuwa ikisemekana kusukwa kumbandua uongozini baada ya upinzani kujumuishwa serikalini.

Pia, alimlaumu Rais akisema ndiye alimwaagiza atoe baadhi ya matamshi tatanishi wakati uhasama wake na familia ya Rais Uhuru Kenyatta ulifikia kilele na jitihada za kumzuia Kinara wa Upinzani Raila Odinga kuingia serikalini.

Akionekana kutotereka, Bw Gachagua alidai vyombo vya serikali vimekuwa vikitumika kuwahangaisha wandani wake kisiasa.

Aliwataja wabunge James Gakuya (Embakasi Kaskazini) na Benjamin Gathiru maarufu kama Meja Donk kati ya wale ambao wamekuwa wakifuatiliwa, mawasiliano yao kunaswa na kuhangaishwa.

Katika kuhangaishwa kwa wawili hao pamoja na wengine, Naibu Rais amekuwa akilaumu Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) pamoja na Mkuu wa Shirika la Ujasusi (NIS) Noordin Haji.

“Kila mtu ambaye nampigia simu, wananasa mawasiliano yangu kisha wanawapigia kuwauliza kile wanachotaka kutoka kwangu ilhali mimi ni Naibu Rais,” akasema.

“Wamemwendea Benjamin Gathiru ambaye alisimamishwa na magari 10 kisha wakachukua simu yake mjini Kenol. Pia walichukua simu ya James Gakuya,” akaongeza.

Aidha, alidai afisa wa zamani wa NIS ambaye alimchukua na kumuajiri baada ya kufutwa kazi kutoka idara ya serikali naye alipigwa risasi akielekea makazi ya Naibu Rais ya Karen.

Rais William Ruto (kulia) na naibu wake Rigathi Gachagua wakagua miradi ya maendeleo eneo la Bondeni, Nakuru hivi majuzi. Picha|Maktaba

Alitaja tukio hilo kama lililokuwa likilenga maisha yake binafsi. Pia alisema aliyekuwa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Nairobi Profesa Stephen Kiama amekuwa akihangaishwa ilhali amekuwa akisimamia chuo hicho vizuri.

Katika kile ambacho kinaonekana kama njia ya kumkabili kabisa Rais Ruto na wandani wake, Bw Gachagua alisema haogopi hoja ya kutimuliwa kwake kuwasilishwa bungeni.

“Nasikia walitaka kuniondoa lakini hawakuwa na idadi tosha. Sasa nasikia kuwa wakiwa na Raila na watu wake kwenye serikali, basi wana idadi tosha ya kuungana na kunitimua,

“Ruto hakuniambia Raila alikuwa anakuja na watu wake kuniondoa mamlakani, alisema walikuwa wanakuja kumsaidia na nikamwaamini. Kwa hivyo, sichukulii suala la kuondolewa mamlakani kwa uzito,” akasema.

Kuhusu kauli kali aliyotoa ya kuzuia upinzani kuingia kwenye ikulu, Naibu Rais alionekana kujitetea akisema alitoa kauli hiyo baada ya kuambiwa na Rais.

“Niliweka mitego mahali kote katika Ikulu na Rais Ruto mwanzoni aliunga mkono mbinu yangu. Nilikuwa naangalia kila siku iwapo mtego wangu ulikuwa umenasa ila nilipoona Rais na Raila walianza kuridhiana niliiondoa. Hapo ndipo Raila aliingia ikulu,” akasema Bw Gachagua.

Kutanua kucha zake dhidi ya serikali, Bw Gachagua alisema hakushirikishwa wakati Seneta wa Kakamega Cleophas Malala alikuwa akibanduliwa kama Katibu wa UDA.

Kutokana na kauli nzito ya kukashifu serikali, wandani wa Rais jana walisema Bw Gachagua amevuka mipaka na sasa wanapanga kumtia adabu hasa kutokana na madai kuwa maisha yake yalikuwa yakilengwa.

Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah na Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa walisema Naibu Rais ni kiongozi mwongo ambaye sasa amefeli viwango vya maadili katika uongozi.

“Ni mwongo na mtu hatari ambaye analenga kuhurumiwa na raia kisha kuisawiri serikali vibaya,” akasema Bw Ichung’wah, mbunge wa Kikuyu ambaye ni hasimu mkubwa wa Naibu Rais.

Naye Bw Barasa alisema iwapo Bw Gachagua ataendelea kuzamisha jahazi la Kenya Kwanza, basi watapeleka hoja ya kutokuwa na imani naye bungeni na kumwondoa madarakani.

“Anajiharibia sana na asipobadilika, tutamwondoa afisini. Kwa sasa tunakabiliwa na maasi ya kisiasa na kiuchumi na hatatuzuia kuyashughulikia masuala haya ili kuipeleka Kenya mbele,” akasema mbunge huyo wa Kimilili.

Kwa mujibu wa mchanganuzi wa kisiasa Profesa David Monda, suluhu kwa sasa ni Rais amtenge Bw Gachagua kabisa katika kuendesha serikali yake.

Profesa Monda anasema Rais anastahili kushirikiana tu na Raila pamoja na Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi.