Rigathi Gachagua sasa ataka Uhuru avunje kimya chake

Rigathi Gachagua sasa ataka Uhuru avunje kimya chake

NA CHARLES WASONGA

NAIBU Rais mteule Rigathi Gachagua amemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuondoka “mafichoni” na kutoa ujumbe wa heri njema kwa Wakenya hata kama hataki kupongeza ushindi wa Naibu wake, Dkt William Ruto katika uchaguzi wa urais.

Akiongea Alhamisi katika Runinga ya Kass TV, Bw Gachagua ambaye ni mbunge wa Mathira anayeondoka alisema unyamavu wa Rais Kenyatta unaibua “wasiwasi”.

“Hata kama hataki kumpongeza Ruto, anafaa kufanya jambo la heshima kwa kutoa ujumbe wa amani na heri njema kwa Wakenya,” akasema.

Aidha, Bw Gachagua alisema sherehe ya kumwapisha Dkt Ruto kama Rais wa Tano wa Jamhuri ya Kenya itaendelea hata bila uwepo wa Rais Kenyatta.

Hata hivyo, kuandaliwa kwa sherehe hiyo ya kumwapisha kutategemea matokeo ya kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais ambayo mgombeaji wa urais wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga, anapanga kuwasilisha katika Mahakama ya Juu, kabla ya Jumatatu, wiki ijayo.\

Akiongea Jumanne, kwa mara ya kwanza baada ya Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchagazi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati kumtangaza Dkt Ruto kuwa mshindi, Bw Odinga alisema ushindi huo sio halali.

“Matokeo yaliyotangazwa na Bw Chebukati ni batili na sisi kama Azimio hatuwezi kutambua,” Bw Odinga akasema.

“Tutafuata njia zingine za kisheria kutafuta haki mahakamani,” akawaambia wanahabari katika jumba la KICC akiandamana na mgombea mwenza wake

Kulingana na matokeo yaliyotangazwa na Bw Chebukati Jumatatu, Agosti 15, 2022 katika ukumbi wa Bomas of Kenya Nairobi, Dkt Ruto alizoa kura 7,176, 141 dhidi ya kura 6,942,930 alizopata Bw Odinga.

Alhamisi Bw Gachagua alisema kutokuwepo kwa Rais Kenyatta katika sherehe ya kumwapisha Dkt Ruto hakutaathiri kwa vyovyote mchakato wa mpito wa mamlaka.

Alitoa mfano wa nchini Amerika ambapo Rais wa zamani Donald Trump, ambaye alishindwa, alichelea kuhudhuria sherehe ya kumwapisha Rais Mpya Joe Biden.

“Kile tunahitaji wakati wa sherehe ya maapisho ni uwepo wa Jaji Mkuu; sio shime – upanga maalum- kwani kifaa hicho hakina umuhimu wowote,” akasema Bw Gachagua.

  • Tags

You can share this post!

Ruto ikulu katika jaribio la kwanza

Tutakupa kazi, Wetangula aambia Uhuru

T L