Makala

Gachagua: Tutawasaka, kuwanasa na kuwahamisha fisi wasumbufu Juja

Na LABAAN SHABAAN August 18th, 2024 1 min read

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amelaumu utekelezaji wa matimbo kwa visa vya fisi kuvamia na kuua wakazi wa Juja, Kaunti ya Kiambu.

Wakati uo huo, Bw Gachagua ametangaza serikali itasaka na kunasa fisi hao wanaohangaisha watu.

“Vifo hivi vinasikitisha. Tunatuma kikosi kukamata fisi na kuwahamisha fisi hao ili wasilete usumbufu. Matimbo yaliyotelekezwa yamekuwa sehemu zao za kujificha,” alisema katika sherehe ya harusi shuleni Juja Preparatory School Jumamosi.

Kadhalika, Naibu Rais alihofia kuwa matimbo hayo pia ni hatari kwa usalama na afya ya wakazi.

Alisema visa vya malaria vinaweza kuibuka kwa sababu yanaweza kuwaumbia makao mazuri ya kuzaa na kuongezeka.

“Matimbo haya yanaweza kusaidia fisi kujificha kabla ya kushambulia watu,” aliendelea. “Maafisa wa usalama watawafukuza wanyamapori na kuangazia visa vya mashambulizi.”

Bw Gachagua alikuwa anamjibu Mbunge wa Juja George Koimburi aliyetaka serikali iingilie kati kuokoa wakazi.

Haya yanajiri baada ya mwanamke mwenye umri wa miaka 52 kuuliwa na fisi mnamo Agosti 7, 2024.

Mashambulizi ya fisi

Baada ya mwanamke huyo kuuliwa na fisi, Shirika la Wanyamapori (KWS) lilizindua awamu ya pili ya ‘Oparesheni Ondoa Fisi Juja.’

Mnamo Januari 2024, KWS ilianzisha awamu ya kwanza ya ‘Oparesheni Ondoa Fisi Juja’ sambamba na kampeni dhidi ya kichaa cha mbwa.

Huu ni mpango unaohusisha wakazi wa Juja ili kumaliza mashambulizi ya fisi.

Oparesheni hiyo ilifaulu kuhamisha fisi 12 kutoka sehemu mbalimbali za Kaunti Ndogo ya Juja.

Maeneo hayo yanajumuisha Munyaka katika Wadi ya Theta, Mwireri eneo la Juja House, Athi, Kikumari Zone, Kimich na Mwalimu Farms.

Aghalabu fisi ni wanyama ambao hujishughulisha usiku lakini pia hushambulia mapema asubuhi.

Makundi ya fisi huzurura katika vijiji vya Nyacaba, Malaba, Athi, Juja Farm, Muthaara, Magomano, Mukuyu na vitongoji vingine maeneo ya Witeithie and Kalimoni.

Licha ya serikali kuanza mikakati ya kuangazia matatizo haya ya mashambulizi, visa hivi vingali vinashuhudiwa.