Habari Mseto

Gachagua: Uhusiano wangu na Ruto ni wa chanda na pete; wanaoeneza uvumi wanikome

May 26th, 2024 3 min read

NA TITUS OMINDE

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amesema ana uhusiano mzuri wa kikazi na Rais William Ruto akisema kuwa Rais Ruto amempa majukumu ya kutosha kuondoa uvumi kwamba uhusiano wao unayumba.

Bw Gachagua ambaye siku chache zilizopita aliwakashifu baadhi ya wanasiasa wa Rift Valley kwa kuingilia siasa za Mlima Kenya alitaja uhusiano wake na Dkt Ruto kama uhusiano wa hali ya juu unaolenga kuimarisha amani na umoja kote nchini.

“Mimi na Rais Ruto tuko katika uhusiano mzuri, kwa kweli Rais amenipa majukumu mengi kama naibu wake na lengo letu kwa sasa ni kuwaunganisha Wakenya wote hasa wale ambao waliingiliwa na hofu wakati wa uchaguzi mkuu uliopita,” akasema Bw Gachagua.

Akizungumza katika Shule ya Msingi ya Matharu katika Kaunti ya Uasin Gishu wakati wa kuchangisha pesa za kusaidia makanisa 15 kutoka eneo hilo, Naibu Rais alitoa wito kwa Wakenya wote kuunga mkono serikali ya Kenya Kwanza.

Bw Gachagua ambaye amekuwa akipiga kambi katika Kaunti ya Uasin Gishu kwa siku tatu zilizopita alisema amejitolea kumuunga mkono Bw Ruto katika azma yake ya kuwaunganisha Wakenya wote.

“Nimekuwa katika kaunti hii kwa siku tatu zilizopita kwa sababu ya maendeleo na kuwashukuru kwa kuunga mkono serikali yetu. Jukumu letu kuu ni kuwaunganisha Wakenya wote ili kuchochea maendeleo,” alisema Bw Gachagua akihutubu katika soko la Burnt Forest baada ya harambee.

Ajabu ni kwamba Bw Gachagua alisimama katika masoko ya Matharu na Burnt Forest ili kuhutubia wakazi kwa ujumbe mmoja tu, ‘tuko pamoja na Rais Ruto’.

Kusimama kwake kulioana na kumbukumbu za kampeni ya uchaguzi mkuu iliyoshuhudiwa mwaka wa 2022.

Wabunge ambao waliandamana na Bw Gachagua waliwakashifu wabunge vijana ambao waliwashutumu kwa kukosa heshima kwa naibu rais kwa kuibua hisia kwamba ndoa kati ya Rais na Naibu wake inaelekea kutibuka.

Wabunge hao walidai kuwa wanasiasa wanaoingilia siasa za Mlima Kenya kwa kumlenga Gachagua ni makundi ambayo yamejilimbikizia mali ndani ya muda mfupi serikalini na wanatumia utajiri huo huo kuibua hisia kwamba wana uwezo wa kudhibiti siasa za Mlima Kenya.

“Wanasiasa wachache ambao wamejipatia mali nyingi tangu tujiunge na serikali, wamenunua magari ya kifahari na sasa wanapiga kelele kwa Wakenya maskini ambao hawana chochote mifukoni mwao kwa hisia kwamba wana uwezo wa kubadilisha siasa za Mlima Kenya,” alisema aliyekuwa Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Laikipia Catherine Waruguru.

Bi Waruguru aliwataka wanasiasa hao kukoma na badala yake wawaruhusu Wakenya maskini kujiendeleza chini ya utawala wa Kenya Kwanza.

“Ikiwa umepata mali ya kutosha kukuridhisha, shukuru Mungu na uachane na nasi tuendelee kusukuma gurudumu la maendeleo,” alisema Bi Waruguru.

Bi Waruguru aliendelea kusema kuwa eneo la Mlima Kenya linaunga mkono kikamilifu uongozi wa Ruto pamoja na naibu wake Gachagua.

Aliwaambia wale wanaofanya siasa za Mlima Kenya kuwa wanacheza na viazi moto mikononi mwao. Alionya dhidi ya kushambulia Naibu wa Rais akisisitiza kwamba eneo la Mlima Kenya liko nyuma ya rais na naibu wake.

“Naibu wa Rais yuko imara katika Mlima Kenya na eneo hilo linamuunga mkono Rais Ruto kwa asilimia 100. Mlima Kenya tuko nyuma ya DP Gachagua kwa asilimia 100; siasa za Milimani ni moto,” akasema Bi Waruguru.

Aliungwa mkono na Mbunge Maalum Joseph Wainaina ambaye aliwataka wanasiasa vijana kwenda polepole.

Bw Wainaina alisema hivi karibuni wataomba viongozi wa makanisa pamoja na wazee wapatanishe viongozi wanaotaka kuleta mifarakano katika chama tawala.

“Tutajaribu tuwezavyo kuleta viongozi na wazee wa kanisa ili watusaidie kurekebisha hali kwa mustakabali wa serikali yetu chini ya uongozi wa Rais Ruto na naibu wake,” alisema Bw Wainaina.

Kati ya wabunge wote sita kutoka Uasin Gishu ni mbunge wa eneo hilo pekee ambaye alikuwepo.

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi alituma mchango wake wa Sh1m.

Viongozi wengine kutoka Uasin Gishu waliokuwepo ni pamoja na Gavana wa Uasin Gishu Jonathan Bii, Seneta Jackson Mandago na Mwakilishi wa Wanawake Gladys Boss Shollei.