Gachie Soccer yasaka kushiriki soka ya Taifa Daraja la Pili

Gachie Soccer yasaka kushiriki soka ya Taifa Daraja la Pili

Na JOHN KIMWERE 

GACHIE Soccer FC ni kati ya vikosi 28 vinavyoshiriki ngarambe ya Nairobi West Regional League (NWRL) muhula huu. Aidha ni miongoni mwa timu zinazoshiriki soka la hadhi hiyo kwa mara ya kwanza. 

Gachie Soccer ya kocha, James Otsibo na Jimmy Imbiakha inalenga kupambana mwanzo mwisho kwenye jitihada za kufukuzia tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki soka ya Ligi ya Taifa Daraja la Pili  msimu ujao.

”Tunafahamu bayana kuwa hakuna mteremko kwenye kampeni hizo lakini tuna imani tunao uwezo wa kujituma kiume na kufanya kweli,” katibu wake, James Karongo alisema na kuongeza kwamba kiwango cha mchezo wao ndicho kiliwapa tiketi ya kupanda ngazi.

KUPANDISHWA NGAZI

Gachie Soccer ni kati ya timu sita zilizopandishwa daraja baada ya kufanya vizuri kwenye mechi za Ligi ya Kaunti chini ya Tawi la FKF, Nairobi West (Magharibi). Vikosi vingine vilivyonasa tiketi ya kushiriki michuano hiyo ni Red Carpet, Re Union, Shallom Yassets, Karura Greens na African Warriors.

Gachie Soccer chini ya nahodha, Joseph Otieno iliyokuwa ikishiriki mechi za Kundi B Ligi ya Kaunti ilipandishwa ngazi baada ya kuibuka miongoni mwa nafasi tatu bora.

”Licha ya kudondosha mechi mbili na kutoka sare mara moja ninaamini nina wachezaji wazuri ambao wakikaza buti watatimiza malengo yetu. Pia ninafahaamu hakuna kisichowezekana bora tutie bidii na kumuaminia Mola.”

Wachezaji wa timu ya Gachie Soccer ambayo imepandishwa ngazi kushiriki kipute cha Nairobi West Regional League (NWRL). PICHA/ JOHN KIMWERE

Kwenye ngarambe ya NWRL Gachie imepangwa Kundi A, linashirikisha vikosi 14 huku likijumuisha timu kali kama Makarios 111 FC (Riruta United), AFC Leopards Youth na Re Union FC kati ya zingine.

Katibu huyo anasema kipute hicho kinatarajiwa kushuhudia ushindani mkali kwani vikosi mbali mbali kama AFC Leopards na Amazon Tigers zimeanza kampeni zao kwa kasi.

Ingawa klabu hii inashiriki mechi za mashinani inajivunia kukuza talanta za wanasoka wachache ambao walibahatika kushiriki soka la hadhi ya juu. Wachana nyavu hao ni Jimmy Mbugua na Anderson Kamau ambao huchezea Tusker F.C  (Ligi Kuu ya BKPL) na M.C.F (Betika Supa Ligi ya Taifa-BNSL) mtawalia.

Meneja huyo anatoa shukran zake kwa James Kaunyo ambaye ameibuka msaada kwao kwa kuwapa usafiri wakati wote wakiwa na mechi za ligi za ugenini. Anatoa wito kwa wahisani wajitokeze na kuungana nao angalau kuwapiga jeki kuendeleza mpango wa kukuza talanta za wachezaji chipukizi.

Timu hii iliyoanzishwa mwaka 2013 inajivunia kushinda taji mwakilishi wa Wadi ya Kihara Super Cup mara tatu. Pia timu ya kikosi hicho kwa wasiozidi umri wa miaka 17 inajivuniaa kubeba bila kufungwa bao hata moja taji la Kariri Njama Super Cup eneo la Kiambaa.

You can share this post!

JAMVI: Mrengo wa Weta, Musalia, Kalonzo, Moi watia Raila,...

Ndoto ya MCAs kupata magari yaanza kuzimika