Galana-Kulalu kukabidhiwa wawekezaji wa kibinafsi

Galana-Kulalu kukabidhiwa wawekezaji wa kibinafsi

NA ANTHONY KITIMO

SERIKALI inajiandaa kukabidhi shamba la unyunyizaji la Galana-Kulalu kwa wawekezaji wa kibinafsi.

Mamlaka ya Kitaifa ya Unyunyizaji (NIA) inayosimamia utekelezaji wa mradi huo wa kilimo, imesema shamba litapeanwa kwa Shirika la Ustawishaji wa Kilimo (ADC) ambalo ndilo husimamia shughuli za kibiashara katika miezi michache ijayo.

Tangazo hilo limetokea siku chache baada ya magavana wa kaunti za Pwani kusema wangependa serikali ya kitaifa iwaruhusu kusimamia shamba hilo la ekari 10,000.

Msemaji wa NIA, Bw Daniel Nzonzo, alisema mamlaka hiyo iko karibu kukamilisha ujenzi wa miundomsingi iliyobaki kabla wakabidhi mradi huo.

“Baada ya kampuni ya Israeli kuacha mradi huu kufuatia mizozano na serikali kuhusu mikataba, kampuni ya Kenya ilitwaa mradi huu huku taasisi nyingine za utafiti zikiendelea kuchunguza mimea inayofaa zaidi kupandwa eneo hili,” akasema Bw Nzonzo.

“Tunafurahi kusema kuwa, mkandarasi yuko karibu kukamilisha na imebaki chini ya asilimia mbili ambayo inaweza kukamilishwa kwa siku chache,” akaeleza.

Aliongeza kuwa, mwekezaji mpya atapewa ripoti kuhusu mimea inayofaa zaidi kupandwa katika shamba hilo baada ya utafiti wote kukamilika.

Bw Nzonzo alisema mkandarasi wa kwanza kutoka Israeli, Green Arava, alikuwa amejenga miundomsingi kwenye ekari 5,100 za shamba hilo.

NIA ilipochukua usukani, ilishirikiana na mkandarasi wa humu nchini, Irico International, ambaye aliitisha Sh800 milioni.

Kiasi hicho ni cha chini ikilinganishwa na Sh5 bilioni zilizokuwa zimeitishwa na kampuni ya Israeli.

Mradi wa Galana-Kulalu ulikuwa mmojawapo na miradi mikuu ya serikali ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta, ambayo ilikosa kutekelezwa kikamilifu kabla aondoke mamlakani.

  • Tags

You can share this post!

Mung’aro sasa afichua ushirikiano na Jumwa

Kenya Kwanza yaanza kutikiswa na mivutano

T L