Habari Mseto

Galleria kufurusha Nakumatt kwa 'kushusha ushawishi wa kibiashara'

February 21st, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

WAMILIKI wa Jumba la Kibiashara la Galleria, jijini Nairobi sasa wanataka kufukuza duka la rejareja la Nakumatt.

Wamiliki hao walisema uwepo wa Nakumatt humo unamaliza biashara kwani duka hilo limeshindwa kununua bidhaa, hivyo kuathiri ulipaji wa mikopo ya Galleria.

Kulingana na Parkside Development inayosimamia jumba la Galleria, Shirika la Kutoza Ushuru (KRA) liliagiza wakodishaji wa nafasi jumbani humo kulilipa moja kwa moja kuhusiana na masalio ya ushuru ya Sh86 milioni yanayodaiwa Galleria na KRA.

Parkside Development ilihoji kuwa hatua hiyo ya KRA imeimalizia mikondo ya mapato, hivyo imekuwa vigumu kulipa mkopo wa benki.

Wamiliki hao wanataka kutwaa nafasi iliyokaliwa na Nakumatt kutokana na kuwa biashara ya duka hilo imeenda chini kwa sababu duka hilo limeshindwa kununua bidhaa, hali ambayo imeathiri biashara za wakodishaji wengine, kwa kushusha ushawishi wa kibiashara eneo hilo.

Kampuni hiyo ilisema tayari imepata mteja mwingine aliye na uwezo wa kuvutia wateja katika jumba hilo, na kuimarisha biashara zingine.

Pia, ilisema kuwa Nakumatt ina deni lake la Sh107 milioni baada ya kushindwa kulipa kodi ya nyumba, na ada zingine.