Michezo

Gani kali, Uholanzi au Uingereza? Uhondo bab’kubwa katika nusu fainali ya pili Euro 2024

Na MASHIRIKA July 10th, 2024 2 min read

DORTMUND, Ujerumani

UholanzI leo Jumatano itakuwa mwenyeji wa Uingereza jijini Dortmund katika nusu-fainali ya michuano ya Euro 2024.

Mechi hii itachezewa Signal Iduna Park, uwanja ulio mkubwa zaidi nchini hapa, ukiwa na uwezo wa kubeba zaidi ya mashabiki 81,000.

Fainali ya mashindano hayo yaliyoanza June 14, itachezwa Jumapili katika uwanja wa Olympic Stadium jijini Berlin.

Kwa upande wa Uholanzi, hii ni fainali ya tano, huku ikijivunia ushindi mara mbili na kushindwa mara tatu.

Ilishindwa na Ureno kwa 2-1 mnamo 2004, na pia ikashindwa na Italia kwa 3-1 kupitia kwa mikwaju ya peanlti.

Katika mechi ya 22, Uingereza imeshinda sita, sare tisa na kushindwa mara saba, lakini katika mechi 10 za mwishoni, Uingereza imeshinda mara mbili katika nane, huku ikipoteza nne na kutoka sare pia mara nne.

Itabidi Uingereza wawe waangalifu dhidi ya washambuliaji matata wa Uholanzi kama vile Cody Gakpo wa Liverpool na Memphis Depay wa Atletico Madrid ambao wamekuwa wakitatiza ngome za wapinzani tangu mashindano haya yaanze.

Dhidi ya Romania katika hatua ya 16-Bora washambuliaji hao walitatiza walinzani mara kwa mara, ingawa safu yao ya ulinzi ikiongozwa na Virgil van Dijk ilionekana kuwa na udhaifu, hivyo akina John Stones, Ezri Konsa, Kieran Trippier na Kyle Walker lazima wawe makini zaidi,
Uingereza wamekuwa wakitengeneza nafasi nyingi, lakini mashuti hawapigi kama ilivyotarajiwa.

Kikosi hicho cha kocha Gareth Southgate lazima kitumie uwezo wa Jude Bellingham na Bukayo Saka ambao mchango wao umekuwa mkubwa.

Uingereza inahitaji kuwa katika kiwango bora zaidi katika safu yao ya ulinzi kwa sababu Waholanzi ni wakali katika safu ya ushambuliuaji.

Timu hizi zilipambana kutoka nyuma na kutwaa ushindi katika robo-fainali baada ya wapinzani wao kufunga kwanza.

Dhidi ya Uswisi, Uingereza ilifunga bao la kusawazisha kupitia kwa mshambuliaji Bukayo Saka wa Arsenal aliyeandaliwa pasi safi kutoka kwa mwenzake wa klabu hiyo, Declan Rice.

Uswisi walitangulia kuona lango dakika ya 75 kupitia kwa Breel Embolo anayechezea klabu ya Monaco nchini Ufaransa.

Mechi hiyo ilimalizika kwa 1-1 hata baada ya muda wa nyongeza, na ikabidi mechi hiyo iamuliwe kupitia kwa mikwaju ya penalti kwa ushindi wa 5-3.

Wakati wa matuta, Uingereza ilifunga yote kupitia kwa Cole Palmer, Jude Bellingham, Bukayo Saka, Ivan Toney na Trent Alexander-Arnold, huku kipa Jordan Pickford wa Uingereza akizuia penalti ya beki Manuel Akanji wa Manchester City.

Uholanzi pia walipambana kutoka nyuma katika robo fainali yao dhidi ya Uturuki baada ya wapinzani wao kutangulia kufunga bao dakika ya 35 kupitia kwa Samet Akaydin.

Vijana hao wa kocha mkongwe Ronald Koeman walirejea uwanjani wakiwa na nguvu mpya na kufaulu kufunga mabao mawili dakika ya 70 na 76 kupitia kwa Stefan de Virji na Mert Muldur.