Gareth Bale afunga bao lake la kwanza la La Liga tangu Septemba 2019

Gareth Bale afunga bao lake la kwanza la La Liga tangu Septemba 2019

Na MASHIRIKA

REAL Madrid na Levante walitoshana nguvu katika mechi ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) iliyokamilika kwa mabao 3-3 mnamo Jumapili uwanjani Ciutat de Valencia.

Mchuano huo ulishuhudia mshambuliaji Gareth Bale akifunga bao lake la kwanza la La Liga tangu 2019.

Bale alifungulia Real ukurasa wa mabao kwa kujaza kimiani krosi ya Karim Benzema katika dakika ya tano kabla ya Roger Marti kusawazisha mambo mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Ingawa Jose Campana aliwarejesha Levante uongozini katika dakika ya 57, juhudi zake zilifutwa na Vinicius Jr aliyesawazisha katika dakika ya 73 kabla ya kupachika wavuni goli la tatu la Real kunako dakika ya 85. Hiyo ilikuwa baada ya Rober Pier kuwafungia Levante bao la tatu kunako dakika ya 79, dakika nane kabla ya kipa wao, Aitor Fernandez kuonyeshwa kadi nyekundu.

Kadi hiyo ilitokana na hatua ya Fernandez kutoka nje ya kijisanduku chake ili kumnyima Rodrygo fursa ya kufunga. Kuondolewa kwake kulishuhudia beki Ruben Vezo akiwajibishwa uwanjani kwa kipindi cha dakika tatu za mwisho za mchezo.

Kuwajibishwa kwa Bale dhidi ya Levante ni ishara kwamba kocha Carlo Ancelotti yuko radhi kufufua makali ya sogora huyo raia wa Wales aliyetumwa na kocha Zinedine Zidane kambini mwa Tottenham Hotspur kwa mkopo mnamo 2020-21 baada ya kutofautiana naye.

Bao la Bale lilikuwa lake la kwanza katika La Liga tangu Septemba 2019 na la kwanza ndani ya jezi za Real tangu Januari 2020.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Washukiwa wawili wa ugaidi wakamatwa Likoni, Mombasa

Familia moja Gatuanyaga yaomba msaada baada ya jamaa wao...