Habari za Kitaifa

Gari la Kiptum lilikuwa katika hali shwari ya kimitambo, uchunguzi wabaini

February 13th, 2024 2 min read

CAROL WAFULA NA JOHN ASHIHUNDU

MATOKEO ya hivi punde zaidi kuhusu uchunguzi wa gari alilokuwa akiendesha Kelvin Kiptum yameonyesha kwamba gari hilo la Toyota Premio lilikuwa katika hali shwari ya kimitambo.

Mwanariadha huyo nyota alifariki pamoja na kocha wake Gervais Hakizamana kwenye ajali mbaya ya barabarani, Jumapili usiku.

Maafisa wa polisi wa kitengo cha trafiki, kuanzia Jumatatu wamekuwa na shughuli nyingi za kuchunguza kwa makini hali ya gari lake hilo lililosababisha ajali hiyo katika eneo la Kaptagat, kwenye barabara ya Eldoret-Eldama Ravine.

Maafisa hao wanataka kujua kilichofanya gari hilo kukosa mwelekeo kabla ya kugonga mti na kusimamia mita 60 kutoka barabarani.

Wakati wa ajali hiyo, Kiptum na kocha Hakizamana waliaga dunia papo hapo, huku abiria Sharon Chepkirui Jepkosgei mwenye umri wa miaka 24 akiponea chupuchupu.

Gari hilo lilibondeka vibaya lakini Sharon aliyekuwa na majeraha madogo madogo alitibiwa Moi Teaching and Referral Hospital (MTRH) na kuruhusiwa kuondoka.

Sharon aliyehojiwa mbele ya wazazi wake katika kijiji cha Kigorot mnamo Jumatatu alieleza jinsi ajali hiyo ilivyotokea.

Mbali na uchunguzi kwenye gari hilo, vile vile ripoti baada ya maiti inatarajiwa kusaidia maafisa hao katika uchunguzi wao kwa kina.

Sharon alieleza polisi jinsi alivyojaribu kumuarifu Kiptum amakinike kabla ya ghafla gari kutumbukia mtaroni.

Watu waliofika mahali hapo mapema pia wanaendelea kuhojiwa kusaidia katika uchunguzi huo.

“Tunaamini ripoti ya uchunguzi itaibua mambo mengi kwa sababu wanaoendesha shughuli hii ni wataalamu wanaoelewa kazi yao vyema. Tafadhali tuacheni tukamilishe uchunguzi wetu ili tuwape ripoti kamili baadaye. Tunahitaji muda wa kutosha kabla kutoa ripoti kamili,” alisema Mulinge.

Jumatatu, waombolezaji walimiminika ilikotokea ajali hiyo huku hali ya huzuni ikitanda nyumbani kwa marehemu katika kijiji cha Chepsamo, Wodi ya Kaptarakwa, Keiyo Kusini, Kaunti ya Elgeyo Marakwet, pamoja na hospitalini Racecourse Hospital uliko mwili wake.

Wanariadha wa tabaka mbali mbali ni miongoni mwa watu waliokusanyika katika sehemu hizo kupata habari zaidi pamoja na kuomboleza na jamii.

Kiptum aliaga wiki moja tu baada ya rekodi yake ya 2:00:35 ya Chicago Marathon kuratibiwa.

Kiptum ameacha mjane, Asenath na watoto wawili wa umri wa miaka saba na minne.