Habari Mseto

Gari la mwanamke aliyeuawa kinyama lapatikana

January 31st, 2019 1 min read

WYCLIFFE MUIA, FRANCIS MUREITHI Na MARGARET MAINA

GARI la mwanamke aliyepatikana ameuawa na mwili wake kutupwa kwenye bwawa eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu, lilipatikana Jumatano.

Gari hilo aina ya Mercedes Benz C200 lilipatikana eneo la Kwamaiko, Githunguri na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Ngewa.

Polisi wanashuku kuwa gari hilo huenda lilitumika na mumewe marehemu, Joseph Kori na mpenziwe Judy Wanbui, kusafirisha mwili wa Mary Kamangara mnamo Jumamosi usiku hadi katika bwawa hilo.

Maafisa wanaochunguza kisa hicho walisema wanaendelea kukusanya ushahidi kutoka nyumbani kwa Judy mtaani Fourways Junction katika barabara ya Kiambu, ambapo marehemu anadaiwa kuuawa.

Jana, huzuni ilitanda katika kijiji cha Kandutura, eneo la Rongai, katika Kaunti ya Nakuru jamaa na majirani wa familia ya Mary walipokusanyika kuomboleza kifo chake.

Mamake marehemu, Virginia Njeri Kamangara alisema bado hajapata nguvu za kusafiri Nairobi kuona mwili wa mwanawe.

Bi Njeri alisema anaamini Mungu atafichua wote waliohusika katika kitendo hicho cha kinyama.

Marehemu Wambui alisomea shule ya msingi ya Kandutura kisha baadaye akajiunga na shule ya upili ya St Columbus eneo la Nakuru kabla ya kwenda Nairobi kusomea kompyuta.

Babake John Kamangara alikuwa mwanasiasa wa chama cha Ford Kenya.