Gari lililojaa bangi lanaswa baada ya kuhusika kwenye ajali ya barabarani

Gari lililojaa bangi lanaswa baada ya kuhusika kwenye ajali ya barabarani

NA KENYA NEWS AGENCY

POLISI walinasa bangi ya mamilioni ya fedha baada ya gari lililokuwa likiisafirisha kuhusika kwenye ajali katika barabara ya Limuru-Kikuyu.

Maafisa wa Kituo cha Polisi cha Tigoni, Kaunti ya Kiambu, walikimbia katika eneo la mkasa kusaidia waathiriwa baada ya kupashwa habari na wakazi.

Lakini walipofika katika eneo la ajali, waathiriwa walikuwa wametimua mbio na kuacha gari lililokuwa limejazwa magunia ya bangi, kulingana na Bw Tom Mwangi, mkazi wa Tigoni.

Kamanda wa Polisi wa eneo la Limuru, Eillin Moraa, alisema kuwa gari hilo dogo lilipoteza mwelekeo na kubingiria kando ya barabara.

“Tuliona wanaume wawili wakitoroka baada ya gari kuhusika kwenye ajali. Tulipoenda kuona kilichowafanya kukimbia tulipata gari limebeba magunia ya bangi,” akasema Bw Alfonse Wekesa, mkazi.

Bi Moraa alisema kuwa gari hilo lilipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Tigoni huku maafisa wa polisi wakiendelea kusaka washukiwa.

“Tumenasa gari hilo na bangi ambayo itatumiwa kama ushahidi. Maafisa wetu wanaendelea na msako dhidi ya washukiwa. Tuna imani watapatikana na kufikishwa kortini,” akasema Bi Moraa.

Miezi miwili iliyopita, gari jingine lilinaswa katika barabara hiyo likisafirisha bangi kutoka Mombasa.

Visa hivi vinaonyesha jinsi matumizi ya bangi yalivyoongezeka nchini hasa miongoni mwa vijana wakiwemo wanafunzi.

You can share this post!

Wakenya wapata hasara umeme ukipotea kote

Familia kortini kupinga hatua ya kuwahamisha

T L