Habari

Gari lingine latumbukia baharini, uokoaji waendelea

December 7th, 2019 1 min read

NA AHMED MOHAMED

GARI moja ndogo limetumbukia baharini katika kivuko cha Likoni Jumamosi alfajiri miezi miwili baada ya gari lingine kuhusika katika mkasa sawa katika kivuko hicho.

Kulingana na Shirika la Huduma za Feri nchini (KFS), bado haijulikani idadi kamili ya watu waliokuwa ndani ya gari hilo wakati wa mkasa huo uliotokea saa kumi na dakika ishirini alfajiri.

Kwenye taarifa, KFS imethibitisha kisa hicho ikisema dereva wa gari hilo alikuwa akiliendesha kwa kasi mno, licha ya maafisa wake kumwashiria apunguze kasi.

Mashirika ya uokoaji yanashirikiana na KFS kutafuta gari hilo Desemba 7, 2019. Picha/ Ahmed Mohamed

“Tuna huzuni sana kuthibitisha kuwa mwendo wa saa kumi na dakika ishirini alfajiri katika upande wa nchi kavu wa kivuko cha Likoni, dereva wa gari ndogo ambalo nambari yake ya usajili haijatambulika baada ya kukata tiketi, aliondoka mbio kwa kasi ya juu na kutumbukia ndani ya Bahari Hindi baada ya kuashiriwa asimamishe gari na maafisa wetu.

“Waliokuwamo hawajatambulika lakini boti za KFS za uokoaji zimeanza shughuli za kusaka gari hilo, zikishirikiana na Jeshi la Majini, polisi na mashirika mengine ya uokoaji,” ikasema taarifa hiyo.

Boti katika shughuli ya kusaka gari hilo Desemba 7, 2019. PIcha/ Ahmed Mohamed

Kwa sasa shughuli ya uokoaji inaendelea huku Wakenya mitandaoni wakishangaa kilichomchochea dereva huyo kuendesha gari kwa kasi akielekea baharini.

Taifa Leo Dijitali itakuleta habari zote kuhusu mkasa huu pindi zinapojiri.

Ni miezi miwili tu tangu mama na mwanawe waangamie baada ya gari lao kutumbukia hapa. Hili hapa ni boti la uokoaji la Jeshi la Majini Desemba 7, 2019. Picha/ Ahmed Mohamed