NA AREGE RUTH
GASPO Women wana kibarua cha kutafuta alama tatu ambazo zitawapandisha hadi nafasi ya pili kwenye jedwali, watakapombana na Kayole Starlets katika mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) ugani GEMS Cambridge, Februari 1, 2023.
Katika mechi hiyo ya raundi ya sita, Gaspo watakuwa wanatafuta ushindi wao wa nne msimu huu wakiwa nyumbani. Kufikia sasa, wameshinda mechi tatu na kuandikisha sare tatu.
Gaspo ambao wana mechi moja kibindoni, wameshikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 12. Alama nne nyuma ya vinara wa ligi Vihiga Queens.
Kwa upande wa kocha wa Kayole Joshua Sakwa, wanaomba Shirikisho la Soka nchini (FKF) kuwapa muda zaidi kujipanga kutafuta hela za matumizi kabla hali haijakuwa mbaya zaidi.
“Hatuna uhakika tutacheza. Lakini tumefanya mazoezi yetu ya mwisho kwa ajili ya pambano hilo. Tunahitaji kiasi cha Sh10,000 kucheza na fedha hizo hatuna hadi sasa. Ikiwa tutapata angalau kidogo, wale wachezaji ambao watajitokeza watacheza tu,” alisema Sakwa.
“Ni ombi letu kwa FKF watupe muda tujipange. Klabu nyingi zinapitia changamoto za kifedha. Hali inaendelea kuwa mbaya zaidi kila kukicha kwa sababu klabu hazina wafadhili,” aliongezea Sakwa.
Kwenye mechi ya awali dhidi ya Trans Nzoia Falcons ambayo walinyeshewa (4-0), timu hiyo ilichezesha wachezaji tisa uwanjani baada ya wachezaji wengine kugoma kutokea.
Kayole kwa sasa wanaburura mkiani bila alama yoyote baada ya kupoteza mechi sita za ligi.
Hata ingawa matokeo ni mabaya kwenye timu hiyo, Kayole wanaongoza kwenye orodha ya timu ambazo zina nidhamu zaidi uwanjani. Hadi kufikia raundi ya sita, wamepata kadi mbili za njano pekee.