Michezo

GASPO Women waliza Kisumu Allstars

May 5th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya GASPO Women ilibamiza Kisumu Allstars kwa mabao 2-1 kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake ya Kenya (KWPL) iliyosakatiwa uwanjani Ruiru Stadium mjini humo.

Nayo Oserian Ladies ililazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na wageni wao na washiriki wapya Nyuki Starlets kwenye patashika iliyochezewa mjini Oserian. Matokeo hayo yanazidi kudhihirisha kwamba kwenye kampeni za msimu huu hakuna mteremko.

Wachezaji wa GASPO Women walishuka dimbani tayari kufunza wenzao jinsi ya kusakata boli. Warembo hao walionyesha mchezo safi na kusimama wima kutokubali kushindwa katika ardhi ya nyumbani. Wincate Kaari alipiga ‘hat trick’ huku Corazone Aquino akiitingia bao moja.

”Nashukuru wachezaji wangu kwa kuonyesha kazi nzuri na kujiongezea ufanisi wa alama zote na kuendelea kujiweka pazuri kukabili wapinzani wengine kwenye kampeni za msimu huu,” meneja wa GASPO Women, Edward Githua alisema. Kufuatia matokeo hayo mabingwa watetezi, Vihiga Queens ingali kifua mbele kwa kuvuna alama 30 sawa na GASPO Women tofauti ikiwa idadi ya magoli.

Kipute hicho kinazidi kushusha msisimko mkali ambapo malkia wa zamani Thika Queens imejikuta njia panda baada ya kupoteza mechi tatu.