Michezo

Gattuso kutua Newcastle Benitez akiondoka

April 23rd, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

JARIDA la Calciomercato nchini Italia limechapisha habari zinazodai kwamba Mkufunzi wa AC Milan, Gennaro Gattuso amepata ofa mpya ya kuifundisha soka Newcastle United msimu wa 2019/20.

Huku hatima yake kama kocha wa mabingwa hao wa zamani ya Ligi ya KLabu Bingwa Barani Ulaya ikiwa bado haijulikani, inadaiwa Gattuso alikutana na ajenti maarufu ya wanasoka Jorge Mendes mjini Milan alikokabidhiwa pendekezo la kuifunza Newcastle msimu ujoa wa 2019/2020.

Kocha wa sasa wa Newcastle maarufu kama The Magpies, Rafael Benitez amekuwa akiendelea na mazungumzo ya kuongezewa kandarasi lakini sasa imebainika mazungumzo hayo yamegonga mwamba na usimamizi wa Newcastle sasa unamtafuta kocha mwingine wa kujaza nafasi yake.

Kandarasi ya Gattuso na AC Milan itatamatika Juni 2021 japo inaripotiwa ana kiu ya kunoa klabu za Uingereza hata kama Milan itamaliza ndani ya nne bora kwenye Ligi ya Serie A na kufuzu kushiriki mechi ya Klabu Bingwa Barani Ulaya(UEFA).