Gavana abuni jopokazi kuchunguza madai hatari kuhusu visa vya uchawi

Gavana abuni jopokazi kuchunguza madai hatari kuhusu visa vya uchawi

Na WYCLIFE NYABERI

GAVANA wa Kisii, James Ongwae amebuni jopokazi litakalochunguza viwango vya imani kwa wakazi wa eneo hilo kuhusu uchawi.

Hatua hii inajiri wiki moja baada ya watu wanne kuteketezwa katika eneo la Marani baada ya kutuhumiwa kumroga mwanafunzi wa shule ya upili.Jopokazi hilo linalohusisha maafisa kutoka serikali ya Kaunti, baraza la wazee wa jamii ya Abagusii, vijana na wafanyabiashara mjini Kisii lina muda wa mwezi mmoja kukamilisha uchunguzi wao.

Akiongea wakati wa kutambulishwa kwa wanachama hao kwa umma jana katika afisi za utawala wa kaunti hiyo, Bw Ongwae alisema tukio la Marani lilimhuzunisha sana, akisema visa kama hivyo havifai kutokea katika jamii ya sasa.

“Nilidhani jambo la mtu kusema fulani ni mchawi lilikuwa limepitwa na ni wakati wa jamii kusonga mbele. Inastaajabisha kuwa mambo kama haya yanatokea. Katika taifa linaloongozwa na sheria, hatuwezi kuruhusu mambo kama haya na wahusika wanafaa kupewa adhabu kali,” gavana akasema.

Kulingana na Bw Ongwae, jopokazi hilo litatumia muda wao mwingi kwenye kisa cha Marani lakini akawataka pia waangazie maeneo mengine ya kaunti.Kamati hiyo itatakiwa kutoa ripoti hususan sababu zinazofanya watu kuwadhania wengine kuwa wachawi, hali ya usalama wa watu wakongwe na sababu zinazowafanya vijana kuwashambulia washukiwa.

Pia watahitajika kutoa mapendekezo namna ya kuepuka visa kama hivyo na utangamano wa wote katika jamii.Familia zilizofiwa na kina ajuza hao zitapata afueni baada ya gavana kutangaza atatoa msaada wa Sh 100,000 kwa kila familia kugharamia mazishi ya kina mama hao.

Pia aliamuru jamaa za waathiriwa kutotozwa ada zozote za mochari na upasuaji wa miili ya wanne hao.Wakati huo huo, polisi wamemhoji mwanafunzi aliyesemekana kuchukuliwa na “wachawi hao” ili kuwasaidia katika uchunguzi.

Ilidaiwa mwanafunzi huyo alitolewa nyumbani kwao majira ya usiku na ‘kutembezwa’ usiku kucha.Jamaa zake walimkuta akiwa hajitambui na asiyezungumza kwa ufasaha.

Baada ya tambiko, mwanafunzi huyo alidaiwa kuanza kuzungumza kwa ufasaha na hapo akawataja aliodai waliomtoa nyumbani kwao.Kamanda wa polisi kaunti ya Kisii Francis Kooli alisema hawatamsaza mtu yeyote aliyehusika na tukio hilo la kinyama.

Tayari washukiwa wanne wamekwisha wasilishwa mahakamani kutokana na uteketezaji wa wakongwe hao.Japo hawakuruhusiwa kujibu mashtaka ya mauaji, Hakimu aliagiza wazuiliwe kwa siku kumi ili afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) itamatishe uchunguzi wake.

You can share this post!

Wajumbe wa Ford-K Bungoma waapa kuchagua Wetangula tena

Migomo shuleni itafutiwe suluhu

F M