HabariHabari za Kaunti

Gavana Achani achemkia wanasiasa wanaotumia basari kujifaidi


GAVANA wa Kwale Bi Fatuma Achani amewaonya wanasiasa dhidi ya kutumia mradi wa basari kujipigia debe kisiasa.

Aliwaonya viongozi kutowahadaa wakazi na kuingiza siasa kwenye suala muhimu la hazina ya elimu.

“Wanasiasa jamani, tuache kuingiza siasa kwenye suala la kielimu. Tusiwahadae wakazi sababu ya manufaa ya kisiasa. Mradi wa basari ni wa kunufaisha wakazi wa Kwale,” alisema Bi Achani bila kutaja mwanasiasa mahususi.

Aliungwa mkono na Naibu wake Bw Chirema Kombo ambaye alisema mradi huo umekuwa katika miaka 10 ya uongozi wa aliyekuwa Gavana wa Kwale Bw Salim Mvurya.

Kulingana na Bw Kombo, mradi huo umeleta maendeleo katika sekta ya elimu eneo hilo.

“Matokeo yanaonekana. Viwango vya elimu vimeimarika sababu ya mradi wa basari ambao pia umesaidia wanafunzi kutofukuzwa shuleni sababu ya ukosefu wa karo. Watoto wetu sasa wana muda mwafaka wa kusoma,” alisifu Bw Kombo.

Naibu Gavana alidokeza serikali hiyo itaendelea kusaidia wanafunzi wa familia ambazo hazijiwezi.

Bi Achani aliwahakikishia wazazi kuwa hakuna mwanafunzi yeyote anayetoka familia maskini atakosa basari.

Aliongeza kuwa wanafunzi wote wanaohitaji basari watanufaika na mradi huo.

Haya yanajiri wakati wanasiasa wanaendelea kukashifiwa kwa kutumia basari kisiasa.

Baadhi ya wanasiasa wamegunduliwa wamekuwa wakiwalazimisha wananchi kuthibitisha kama ni wapigakura maeneo husika kabla ya kupewa basari.

Mjadala unaendelea nchini kuhusu kubuniwa kwa njia mpya ya utoaji basari ili kuleta mageuzi muhimu katika sekta ya elimu.