Gavana Achani alalamikia MCAs kuchelewa kuidhinisha mawaziri wake

Gavana Achani alalamikia MCAs kuchelewa kuidhinisha mawaziri wake

SIAGO CECE Na JURGEN NAMBEKA

MVUTANO kati ya gavana wa Kwale, Fatuma Achani na madiwani wa kaunti hiyo kuhusiana na mawaziri aliowateuwa, umewaacha wakazi kwenye njia panda.

Huku madiwani hao wakinuia kusitisha vikao vya bunge kwa ajili ya likizo, orodha ya mawaziri aliyowasilisha Bi Achani bado haijaidhinishwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kituo cha ubaharia katika kaunti hiyo, Bi Achani alilalamikia kutopitishwa kwa orodha ya mawaziri, aliyowasilisha kwa bunge la kaunti hiyo.

“Kazi haiendelei kama sina mawaziri. Mnipitishie mawaziri kazi iendelee. Nilipeana orodha kitambo. Msipopitisha orodha hiyo, kazi mliyochaguliwa na wananchi kufanya haiwezi kufanyika,” alisema Bi Achani.

Kulingana naye, madiwani walikuwa wamechelewa kupitisha mawaziri wake, na alikuwa akihudumu bila mawaziri.

“Makatibu wameteuliwa hivi majuzi, siku mbili washaapishwa. Mimi mwanifanya kusubiri miezi miwili, nikifanya kazi na mawaziri washikilizi,” aliongeza Bi Achani.

Kulingana na mkazi wa Kwale Bw Richard Onsongo ambaye hufuatilia masuala ya kaunti hiyo kwa karibu, kuchelewa huko ni njama ya kuhangaisha gavana Achani.

“MCAs hawa wamechelewa kuwapitisha mawaziri na watatufanya wakazi kukosa huduma endapo wataenda mapumzikoni bila kuwapitisha. Wameshindwa na kazi na ni njama ya kuyumbisha dau la gavana Achani,” alisema Bw Onsongo.

Kulingana naye, MCAs hao wamekuwa wakitumia muda wao afisini kuzuru sehemu mbalimbali za nchi, badala ya kutekeleza wajibu wao.

“Iwapo kuna mawaziri ambao hawajafuzu kuhudumia wananchi, sio wote katika orodha hiyo ambao hawajafuzu. Ni vyema wapitishe waliofuzu na kuwakataa wale ambao hawajafuzu kuhudumu,” aliongeza Bw Onsongo.

Bw Onsongo pia alieleza kuwa, iwapo MCAs hao watafeli kupitisha mawaziri hao ipasavyo, watachukua hatua ya kutafuta saini kutoka kwa wakazi kumwomba Rais William Ruto kuvunja bunge hilo, na uchaguzi mwingine kufanyika.

  • Tags

You can share this post!

Polisi wanasa washukiwa wawili wa ujambazi

Mauzo: Ngamia wachelewesha meli kuondoka bandarini Lamu

T L