Habari MsetoSiasa

Gavana anukuu Biblia huku akigura kundi la Ruto

December 17th, 2019 1 min read

Na NDUNGU GACHANE

VUGUVUGU la kisiasa linalomuunga mkono Naibu wa Rais William Ruto, maarufu kama ‘Tangatanga’ limepata pigo kubwa la kisiasa baada ya Gavana Mutahi Kahiga wa Kaunti ya Nyeri kutangaza kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta.

Bw Kahiga alisema ni Mungu pekee anayejua yule ataiongoza nchi baada ya Rais Kenyatta kustaafu 2022.

Gavana huyo amekuwa mshirika wa karibu wa Dkt Ruto kwani amekuwa akihudhuria hafla zake mbalimbali katika eneo hilo.

Lakini akinukuu Biblia, Bw Kahiga alimwambia Dkt Ruto kusubiri wakati huo ufike, huku akiwarai viongozi wa Mlima Kenya kukomesha kampeni za mapema.Alisema badala yake, wanapaswa kumuunga mkono Rais Kenyatta kutimiza ajenda zake za maendeleo.

“Zaburi 75: 6 inasema kwamba msijisifu, kwani Mungu ndiye humwinua mwanadamu amtakaye. Ndiye mwenye uwezo wa kumwinua ama kumshusha mwanadamu. Tunaweza kutumia muktadha huo kurejelea uchaguzi mkuu wa 2022,” akasema Bw Kahiga.

Hatutaki siasa katika eneo la Mlima Kenya. Lazima tutafute njia ya kuzima malumbano yaliyopo. Hatupaswi kupigana kwa sababu ya mwanamume anayemtafutia riziki mke na watoto wake, lakini si kuangazia maslahi yetu.

Tuna jukumu la kukamilisha kazi ambayo Rais anatutaka tumalize. Tunaweza kulifaidi eneo hili sana kwa miaka mitatu iliyobaki ikiwa tutaacha siasa na kumuunga Rais Kenyatta mkono,” akasema.

Gavana huyo alikuwa ameandamana na mwenzake Anne Waiguru wa Kirinyaga kwenye hafla maalum ya kumtawaza Askofu Francis Kariuki wa kanisa la AIPCA Dayosisi ya Gatanga, Kaunti ya Murang’a.

Bi Waiguru pia amewahi kuonekana kama mwandani wa Ruto kabla kubadili msimamo wake kushabikia handsheki ya Rais Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Bw Kahiga alisema kuwa eneo hilo halipaswi kukubali kugawanywa kisiasa.Kauli yake inajiri huku serikali ikizidisha vita dhidi ya ufisadi.

Kufikia sasa, magavana watatu wamezuiwa na mahakama kuingia katika afisi zao hadi kesi dhidi yao kuhusu ufisadi zisikizwe na kuamuliwa.