Habari MsetoSiasa

Gavana aomba Rais msamaha kwa niaba ya wabunge

March 12th, 2019 2 min read

Na JEREMIAH KIPLANGAT

GAVANA wa Elgeyo Marakwet Alex Tolgos jana aliwapuuzilia mbali viongozi wa Rift Valley ambao wamemshambulia Rais Uhuru Kenyatta kuhusiana na vita dhidi ya ufisadi, akisema huo ni utovu wa heshima kwa kiongozi wa taifa.

Huku akiwa kiongozi wa kwanza wa cheo cha juu, kutoka neo hilo, kutofautiana na wenzake kuhusu suala hilo, Bw Tolgos alimwomba radhi Rais kuhusiana na matamshi makali yaliyotolewa mwishoni mwa juma na baadhi ya viongozi hao kuhusu uchunguzi unaoendelea wa sakata ya ujenzi wa mabwawa mawili katika kaunti hiyo.

Mwishoni mwa wiki baadhi ya wabunge walitishia kuongoza maandamano dhidi ya serikali ikiwa Rais Kenyatta atadhubutu kusitisha ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer kwa sababu ya madai ya wizi wa Sh21 bilioni za kufadhili miradi hiyo.

Wabunge hao; Daniel Rono (Keiyo Kusini), Kangogo Bowen (Marakwet Mashariki), William Kisang (Marakwet Magharibi) na Mbunge Mwakilishi wa kaunti hiyo Jane Kiptoo walisema wako tayari kuanzisha uasi dhidi ya utawala wa Rais Kenyatta ikiwa miradi hiyo itasimamishwa kwa sababu ya uchunguzi unaoendelea kuhusu sakata hiyo.

Walidai kuwa uchunguzi huo unachochewa kisiasa na unalenga watu kutoka jamii moja, lengo likiwa ni kuhamisha miradi hiyo kutoka kaunti hiyo hadi kwingineko.

Lakini jana, Gavana Tolgos alisema kuwa serikali ya kaunti yake haiungi mkono vitisho hivyo, akisema kauli za wabunge hao haziwakilishi hisia za wakazi.

“Kwa niaba ya watu wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet, tungependa kumwomba msamaha Rais Uhuru Kenyatta kuhusiana na matamshi yaliyotolewa na wabunge wanne na madiwani kadhaa wakidai kuongea kwa niaba ya watu wa Elgeyo Marakwet. Matamshi hayo ni ya wabunge hao kama watu binafsi na hayawakilishi maoni ya watu wa Elgeyo Marakwet na uongozi wake,” Gavana alisema.

Bw Tolgos pia ametofautiana na Seneta wa kaunti hiyo Kipchumba Murkomen kuhusu namna uchunguzi wa sakata hiyo unaendeshwa akisema viongozi hao wanafaa kuonyesha heshima kwa Rais badala ya kutoa vitisho kupitia vyombo vya habari.

“Ikiwa wabunge wa Elgeyo Marakwet wamekasirishwa na uchunguzi unaoendelea kuhusu sakata ya mabwawa ya Arror na Kimwarer, wanafaa kutoa hisia zao kwa heshima. Na ikiwa wamechukizwa na muafaka kati ya Rais na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga wanapaswa kufuata utaratibu kuwasilisha malalamishi yao,” Bw Tolgos akaongeza.