Habari MsetoSiasa

Gavana aomba serikali yake ivunjwe

July 2nd, 2019 1 min read

Na LUCY MKANYIKA

GAVANA Granton Samboja ameanzisha mchakato wa kuvunja serikali ya kaunti yake ya Taita Taveta.

Hii ni kufuatia malumbano ya bajeti baina yake na madiwani.

Bw Samboja alitia saini stakabadhi ambayo ni maombi yatakayotumwa kwa Rais Uhuru Kenyatta ili kumwezesha kuvunja serikali hiyo.

Alisema kuwa yeye pamoja na mawaziri wake watazunguka katika kaunti hiyo kuchukua saini 18,000 za wenyeji ili kutuma maombi hayo kwa Rais Kenyatta.

Haya yanajiri baada ya gavana huyo kukataa kuidhinisha makadirio ya bajeti ya 2kutokana na MCAs kujitengea Sh830 milioni kwa hazina ya wadi katika bajeti ya jumla ya Sh5.4 bilioni.

Kila wadi ilitengewa Sh41.5 milioni kwa miradi mbalimbali.

Bw Samboja alisema kutokana na hatua hiyo, idara mbalimbali za kaunti zimesalia na fedha kidogo za kufanya maendeleo.

“Sababu kuu ya kufanya maamuzi haya ni kulinda kaunti yetu dhidi ya madiwani ambao wamekuwa kikwazo cha maendeleo,” akasema.

Aliongeza kuwa bunge la kaunti hiyo limedai kutengewa bajeti ya Sh670 milioni kinyume cha sheria.

Bw Samboja alisema kuwa matakwa ya wawakilishi hao ni kupewa asilimia 15 ya bajeti ya kaunti hiyo.

Alisema kuwa wawakilishi hao wamepanga kumng’oa mamlakani kwa kushikilia msimamo wake wa kutotia saini bajeti iliyopitishwa na bunge hilo wiki jana.

“Mawaziri wangu wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu mno. Wengine wanatukanwa na hawa madiwani na kutishiwa kuwa watatimuliwa,” akasema.

Kwa upande wao, madiwani walipuuzilia mbali madai ya Gavana Samboja.

Wawakilishi hao walisema kuwa hawatatishiwa na mchakato wa kuvunja serikali ya kaunti hiyo.

Wakihutubia wanahabari, madiwani hao wakiongozwa na spika Meshack Maghanga, walisema kuwa upande wa mawaziri umekuwa na njama ya kufuja fedha za umma.

Alisema kuwa baadhi ya idara zilitenga mamilioni ya fedha kwa minajili ya kuzifuja.