Habari MsetoSiasa

Gavana aonya wakazi wajihadhari na wasafiri

July 20th, 2020 1 min read

Na PHYLLIS MUSASIA

GAVANA wa Nakuru, Bw Lee Kinyanjui ametahadharisha wakazi wa kaunti hiyo kuwa waangalifu wakati huu ambapo watu wengi wanapitia kaunti hiyo wakisafiri kuelekea kwingine.

Aliwataka wakazi wa Nakuru kuwa makini ikizingatiwa kuwa kaunti hiyo inatumika kwa safari za kuelekea sehemu nyingi nchini.

Kulingana naye, wakazi wengi wameonekana kupuuza kanuni zilizotolewa na wizara ya afya na wamerejelea mmaisha yao ya kawaida.

Aidha, wanaohudhuria mazishi hawazitangatii maagizo ya kujikinga na maambukizi.

“La kusikitisha ni kwamba, huenda tukafika kilele za maambukizi hivi karibuni iwapo hatutazingatia sheria zilizowekwa. Ni jukumu la kila mmoja kujikinga na kuwalinda walio karibu naye,” akasema.

Gavana huyo amehofia kuwa huenda msimu wa baridi ukachangia maambukizi zaidi ya virusi vya corona nchini.

Kulingana naye, mwezi huu wa Julai huwa msimu wa baridi kali na huenda watu wakaugua ugonjwa wa Covid-19 na kudhani ni homa ya kawaida.

Akizungumza kwenye kikao na wanahabari, Gavana Kinyanjui alisema baridi kali ya mwezi huu wa Julai utazua changamoto nyingi kuhusiana na jinsi ya kudhibiti maambukizi.

“Wakati huu wa msimu wa baridi, huenda ugonjwa wa Covid-19 ukadhaniwa kuwa homa ya kawaida. Nanawasihi watu wote kuwa makini na kutafuta matibabu haraka iwapo watahisi wanaugua,” akasema Bw Kinyanjui.

Alisema kuwa ni rahisi kwa mtu yeyote ambaye anaugua virusi vya corona bila kuonyesha dadlili kusambaza virusi hivyo kwa watu wengine haswa kupitia safari ambazo zinazidi kushuhudiwa.

“Familia nyingi wakati huu zipo katika hali ya hatari kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19 kufuatia wageni ambao wanazidi kufika katika maeneo ya mashinani wakiwa wametoka miji ilioathirika,” akasema.