Habari za Kaunti

Gavana apapurwa kwa kudhibiti muguka ‘nusunusu’

June 7th, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

BAADHI ya wanajamii Kaunti ya Lamu wamemchemkia Gavana Issa Timamy kwa kile wanachodai kuwa ni kudhibiti muguka na miraa ‘nusunusu’.

Haya yanajiri baada ya Gavana Timamy juma hili, kuibuka na masharti matatu ya kudhibiti biashara ya muguka na miraa kote Lamu.

Masharti hayo ni pamoja na miraa na muguka kutouzwa kwenye vishoroba, vichochoro au njiani kwenye miji yote ya Kaunti ya Lamu.

Marufuku ya pili ni kwamba biashara ya miraa na muguka isifanyiwe karibu na maeneo ya ibada kama vile misikitini na makanisani na pia kwenye taasisi za elimu, vikiwemo vyuo na shule.

Tatu, Bw Timamy alipiga marufuku wanabiashara wa miraa na muguka dhidi ya kuuzia bidhaa hiyo watu walio chini ya miaka 18 (yaani watoto).

“Masharti matatu haya tunayoyatekeleza mara moja yananuia kudhibiti uuzaji na matumizi ya muguka na miraa kwenye kaunti yetu. Masharti mengine zaidi yatafuata,” akasema Bw Timamy.

Punde baada ya kiongozi huyo wa kaunti kutangaza masharti hayo, wananchi waliohojiwa walionekana kutoridhishwa au kutosheka na maamuzi ya Gavana wao, wakichacha kuwa ni bora angepiga marufuku kabisa kuendelezwa kwa biashara ya miraa na muguka Lamu.

Mwanamume akibeba mguka. PICHA | MAKTABA

Bw Abdalla Ali, ambaye ni mkazi wa kisiwa cha Lamu, alieleza jinsi miraa na muguka inavyoleta athari mbaya na hata kuisambaratisha jamii kiuchumi na kimaendeleo.

Bw Ali alieleza jinsi ambavyo miraa na muguka husababisha wakazi wanaoitafuna kutolala ambapo hata baadhi wamegeuka kuwa machizi wakichana miraa mchana kutwa na usiku kucha.

“Tulitarajia kumuona Gavana Timamy akichukua mkondo wa magavana wenzake wa Pwani kama wale wa Mombasa, Taita Taveta na Kilifi ambao walijitokeza kupiga marufuku kikamilifu biashara ya muguka na miraa. Sisi hapa Lamu tungependelea sana kutoona miraa na muguka ikiingia. Yaani hatuitaki kabisa,” akasema Bw Ali.

Bi Fatma Abubakar aliilinganisha hatua ya Gavana Timamy ya kudhibiti uuzaji wa miraa na muguka vichochoroni au kwenye maeneo ya umma, shuleni, vyuoni, misikitini, makanisani na kuzuia uuzaji dhidi ya walio chini ya umri wa miaka 18 kuwa sawa na kupiga marufuku biashara hiyo nusunusu.

Bi Abubakar alisema hata kabla ya Bw Timamy kuchukua hatua ya kupiga marufuku uuzaji wa miraa na muguka vichochoroni na njiani mijini, tayari biashara hiyo ilikuwa ikinogeshwa vibandani, madukani na hata ndani ya majumba ya wakazi hasa kwenye miji maarufu kama vile ule  wa kale wa Lamu, Mpeketoni, Hindi, Mokowe, na Witu.

“Yaani gavana wetu ni kama hajafanya lolote. Ukipiga marufuku uuzaji wa muguka na miraa njiani na vichochoroni mijini, hilo linamaanisha umeruhusu iendelee ndani ya majumba, madukani na kwenye vioksi. Sisi msimamo wetu ni miraa na muguka ikataliwe kabisa kuingizwa na kuuzwa Lamu. Tumechoka kuona wanaume na vijana wetu wakiangamia,” akasema Bi Abubakar.

Bi Amina Yusuf alikosoa hatua ya Bw Timamy ya kutopiga marufuku kabisa biashara hiyo Lamu, ambapo alihoji ni vipi shinikizo za kila mara za wanasiasa wa eneo hilo za kutaka watu kutia juhudi kuzaana na kuongeza idadi yao zitafaulu.

Kulingana na sensa ya mwaka 2019, Lamu ina idadi ya watu ambao kwa jumla ni 143,920 pekee.

Hilo kila mara limekuwa likiwasukuma wanasiasa, hasa Seneta wa Lamu Joseph Githuku Kamau, kuwarai wakazi wa kaunti hiyo kutia juhudi kuzaana kwa wingi ili idadi ya watu ipande.

Seneta wa Lamu Joseph Githuku Kamau. PICHA | KALUME KAZUNGU

Katika harakati za kuhimiza wananchi wa Lamu kuzaana, Bw Githuku amekuwa na kampeni maalum ya kuzunguka na kuwatunukia wajawazito Sh500 kama njia mojawapo ya kutambua juhudi zao.

Seneta huyo anaamini idadi ya watu ikiongezeka, Lamu itaweza kutengewa mgao wa kutosha wa fedha kila mwaka, hivyo kufanikisha miradi zaidi ya maendeleo eneo hilo.

Ikumbukwe kuwa Lamu ndiyo kaunti inayopokea mgao wa chini zaidi wa fedha kila mwaka kutoka kwa hazina ya kitaifa ikilinganishwa na kaunti zote 47.

Katika mwaka wa kifedha wa 2024/2025 kwa mfano, mgao wa Lamu kutoka kwa serikali kuu ni Sh3.2 bilioni pekee.

“Muguka na miraa imewasukuma vijana wengi kudinda kuoa. Yaani hawataki kamwe majukumu ya kifamilia. Kwa wale waliooa nao wamekuwa goigoi, hivyo kukwepa kulala nyumbani, ambapo wanatumia muda mwingi wakiwa maskani kuchana. Hawana wasaa wa kulala na wake zao. Wake nyumbani wanalalamika kunyimwa haki yao ya kitandani. Tutazaana vipi hadi kuongezeka? Miraa ingepigwa marufuku kabisa Lamu,” akasema Bi Yusuf.

Bw Samson Kamande, mkazi wa Hindi, alisema alimtarajia Bw Timamy kwamba angalau angepandisha kodi ya magari yanayosafirisha miraa na muguka na pia ile ya wachuuzi wenyewe wa biashara hiyo wanaohudumu Lamu ili kuwavunja moyo.

Vifurushi vya miraa. PICHA | MAKTABA

“Gavana wetu hata angechukua hatua kama ile ya Gavana wa Kwale, Bi Fatma Achani. Apandishe bei ya kodi kwa malori yanayoingiza miraa Lamu hadi wanaotekeleza biashara hiyo washindwe kumudu gharama hiyo ya juu ya kodi. Masharti aliyotoa gavana wetu ni rahisi sana kutimizwa na hawa wasambazaji na wachuuzi wa muguka na miraa,” akasema Bw Kamande.

Huku malalamishi hayo yakijiri, wanabiashara na wachuuzi wa miraa na muguka kote Lamu walifurahia masharti ya Gavana Timamy, ambapo wengine walimshukuru kwa kile walichosema ni kuwazingatia.

Wanabiashara hao hata hivyo waliwakosoa wazazi kwa kuchangia muguka na miraa kutumiwa na watoto wadogo eneo hilo.

Aidha walimuomba Bw Timamy kuwajengea vibanda vya kuuzia miraa na muguka mijini hasa baada ya kuamuru wafurushwe vichochoroni na mabarazani.

“Wazazi wa Lamu wajilaumu wenyewe. Wao ndio wanaowatuma watoto wao mafungu ya miraa na muguka kuwanunulia na kuwapelekea nyumbani kuchana. Hilo limewasukuma watoto wadogo kabisa kuishia kuingilia uraibu kama wazazi wao. Wazazi waache malezi mabaya kwa watoto wao,” akasema Bw Vitalis Munene, mchuuzi wa miraa kisiwani Lamu.