Habari MsetoSiasa

Gavana apiga muuguzi kalamu kwa kuchelewa kufika kazini

January 20th, 2020 1 min read

Na OSCAR KAKAI

MUUGUZI wa kituo cha afya katika Kaunti ya Pokot Magharibi, alifutwa kazi jana Gavana John Lonyangapuo alipozuru hapo ghafla na kumpata hayuko kazini.

Gavana aliwasili katika zahanati hiyo ya Losam na kumuachisha kazi mhudumu huyo kwa kumkosa kazini.

Zahanati hiyo iko katika kaunti ndogo ya Pokot Kati, karibu na mpaka wa Kenya na Uganda.

“Hii ni saa mbili kasoro dakika tano asubuhi na jamaa huyo hayupo kazini. Jamaa huyo anafanya kazi kama mwalimu wa shule ya msingi ambaye huenda nyumbani kila wikendi.

“Huu ni mchezo. Ugonjwa haujui wikendi. Kazi imepotea mara moja. Jumatatu asikanyage hapa kwa sababu amependa nyumbani kwake kuliko kazi. Huwezi kufunga kituo cha serikali hivi,” akasema.

Gavana huyo alisema kuwa muuguzi huyo alipoteza kazi kwa kutelekeza wajibu wake huku wagonjwa wa kijiji hicho wakiendelea kuumia.

“Hatuwezi kukubali watu ambao wanakosa kufanya kazi ilhali wagonjwa wanaumia baada ya kuja hapa na kupata hakuna muuguzi.Hili ni jambo la kuhuzunisha kuhusu mtu ambaye analipwa fedha nyingi na serikali kupeana huduma,” aliongeza.