Habari MsetoSiasa

Gavana ataka mahari sawa kwa mabinti waliosoma na wasiosoma

December 22nd, 2019 2 min read

Na ALEX NJERU

GAVANA wa Tharaka-Nithi Muthomi Njuki amependekeza kwamba Baraza la Wazee wa Njuri Ncheke lipitishe uamuzi utakaofanya wasichana waliosoma na wasio na kisomo kulipiwa kiasi sawa cha mahari wanapoolewa.

Hii ni baada ya malalamishi kuzuka kwamba baadhi ya familia huomba kulipwa mahari ya juu, zikidai kwamba zilitumia fedha nyingi kuwaelimisha binti zao waliofuzu na shahada mbalimbali kutoka vyuo vikuu au vyuo anuwai.

Hali hii imechangia vijana wengi kushindwa kuoa na akasisitiza kuwa mila na tamaduni za jamii ya Ameru zinatoa mwongozo bora wa mahari ambayo familia ya mwanaume anayetaka kuoa inafaa kulipa.

“Bila kuzingatia kama wameelimika au la, mahari kwa wasichana wote inafaa kuwa sawa,” akasema Bw Njuki hapo jana mjini Chuka.

Kiongozi huyo alidai kwamba kulingana na desturi ya jamii ya Ameru, familia ya mwanaume huhitajika kulipa mahari kwa kutoa mifugo, pombe ya kitamaduni na asali kama njia ya shukrani kwa familia ya msichana badala ya maelfu ya fedha yanayoitishwa na wazazi wa kizazi cha sasa.

Alidai baadhi ya wazazi sasa wamegeuza ulipaji mahari kama kitega uchumi huku wakikosa kutilia manani iwapo mwanaume anayeoa mwanao amesoma au hakusoma.

“Kama wazazi tunafaa tukome kufanya biashara na wasichana wetu. Tunafaa kuwaombea na kuwabariki wanapoanzisha familia zao,” akaongeza mbunge huyo wa zamani wa Chuka Igambang’ombe.

Mnamo Oktoba mwaka huu, wazee wa Njuri Ncheke wakiongozwa na Katibu Mkuu wa baraza hilo, Bw Josphat Murangiri, walikutana na Gavana wa Meru, Bw Kiraitu Murungi kisha wakakubaliana kutunga sheria ambazo zitasawazisha mahari kwa wasichana wa kaunti za Tharaka-Nithi na Meru.

Wazee hao pia walitambua kwamba wazazi wamekuwa wakitaka mahari ya juu kabla ya mabinti zao kuolewa, hali ambayo imewazuia vijana wengi wa kiume kuingia kwenye asasi ya ndoa na kuanzisha familia zao.

Wakati wa mkutano huo, Bw Murungi aliwatahadharisha wazazi dhidi ya kuitisha mahari ya juu na kuvuruga maisha ya baadaye ya watoto wao wa kike.