Gavana ataka uchaguzi uahirishwe

Gavana ataka uchaguzi uahirishwe

Na ALEX NJERU

GAVANA WA THARAKA NITHI Muthomi Njuki ametoa wito kwa serikali kuu kutenga pesa za kutosha kupambana na janga la njaa na itafakari kuhusu kuahirisha uchaguzi mkuu wa 2022 iwapo ukame utaendelea kushuhudiwa nchini.

Bw Njuki alisema pesa ambazo zimetengewa uchaguzi huo zinafaa zitumike kununua vyakula vya msaada ili kuwaauni Wakenya wanaokabiliwa na njaa.

Alizungumza hayo katika soko la Nairobi Ndogo katika eneobunge la Chuka/Igambang’ome baada ya kusambaza hundi ya Sh23 milioni kwa makundi 18 ya kibiashara kupitia mradi wa Kilimo na Hali ya Anga (KCSAP). Bw Njuki alisema ingawa Rais Uhuru Kenyatta alitangaza ukame kama janga la kitaifa mapema mwaka huu, juhudi za kutosha hazijafanywa kuhakikisha kuwa walioathirika wanafikiwa kwa kupewa msaada wa vyakula na maji.

“Lengo la kwanza la serikali linafaa kuwa kupambana na njaa ambayo inaendelea kuwaathiri Wakenya wengi. Uchaguzi na mahitaji mengine yanafaa yaje baadaye,” akasema. Bw Njuki. Mwanasiasa huyo alisikitika kuwa wanasiasa wamekuwa wakiendelea na kampeni zao ilhali kuna baa la njaa, akitaka Wizara ya Ugatuzi kwa ushirikiano na Baraza la Magavana (COG) ziibuke na mpango wa kuwafikia wanaohitaji msaada wa vyakula kwa dharura.

Alilalamika kuwa kaunti yake si kati ya yale kwenye orodha ya yanayofaa kupokea msaada huo licha ya Mamlaka ya Kupambana na Ukame (NDMA) kuonyesha kuwa maelfu ya wakazi wanakabiliwa na njaa.Bw Njuki alisema mvua ilinyesha mara ya mwisho Tharaka na Igambang’ombe mnamo Machi na wakazi hajapata mavuno ya kutosha.

You can share this post!

JAMVI: Ruto anasa ‘samaki’ mkubwa Gavana Mvurya...

Zaidi ya Sh1.5M zachangiwa Congo Boys FC

T L