Siasa

Gavana ataka wachochezi waanikwe

December 22nd, 2020 2 min read

Na DENNIS LUBANGA

GAVANA wa Kaunti ya Uasin Gishu, Jackson Mandago, amewataka wakazi kutoa ripoti kwa vyombo vya usalama kuhusu mienendo ya watu wanaowashuku kupanga kuchochea fujo taifa linapojiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022.

Akiongea jana katika Ukumbi wa Kijamii wa Eldoret wakati wa kutawazawa kwa diwani wa wadi ya Kiplombe Ramadhani Ali kuwa msemaji wa Waluhya kaunti hiyo, Mandago alisema masuala ya usalama yanapasa kuchukuliwa kwa uzito.

Alisema wakazi na Wakenya kwa ujumla sharti wahakikishiwe usalama wao hasa wakati huu ambapo joto la kisiasa limeanza kupanda.

“Ikiwa kuna watu katika kaunti hii ambao wanapanga kuzua fujo na mnawajua, msinyamaze. Mkisikia kwamba kuna watu wanaofanya mikutano ya siri kwa lengo la kuzua taharuki, tafadhali toa habari hizo kwa maafisa wa usalama,” akasema Gavana Mandago.

Alionya kuwa wale ambao wanaweza kuwa na habari kuhusu watu kama hao na wakanyamaza, watachukuliwa hatua kali.“Ikiwa una habari na hutaki kuwapasa maafisa wa polisi, hiyo ina maana kuwa wewe ni mshirika wa wahalifu. Bila shaka hatua kali itachukuliwa dhidi yako,” Bw Mandago akasema.

“Tuwe makini, tutoe habari kwa maafisa wa polisi na wale wa Nyumba Kumi,” akaongeza.

Gavana Mandago alisema yeye pamoja na viongozi wa eneo hilo wako tayari kupalilia amani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

“Utulivu unaoshuhudiwa hapa Uasin Gishu ndio tunataka uwe sehemu zote nchini. Tunataka kuelekea uchaguzi tukiwa taifa lenye amani,” akaeleza.Kuhusu suala la mchakato wa BBI, Gavana Mandago aliitaka kamati simamizi ya mchakato huo kuhakikisha kuwa wananchi wamepata nakala za ripoti hiyo ili waisome kabla ya kufanya uamuzi kuihusu.

“Hatufai kupoteza wakati kuhusu suala hili. Wananchi hawajapewa nakala za ripoti hii. Wanaoiunga mkono na wale wanaoipinga wanafaa kuketi chini na kukubaliana ili tuweze kupiga kura kwa mapendekezo hayo na tusonge mbele,” akaeleza.

Naibu Gavana Daniel Chemno alionya kwamba ikiwa ripoti ya BBI itapitishwa itawabebesha Wakenya mzigo mzito kwa sababu imependekeza kubuniwa kwa nyadhifa zaidi za uongozi na ubunge.

“Ikiwa ripoti ya BBI itapitishwa ina maana kuwa tutakuwa na wabunge 600. Tutakuwa na bunge kubwa kuliko ile ya Amerika. Hii ndio maana tunapendekeza kuwe na mazungumzo kuhusu suala hili,” akasema.