Habari MsetoSiasa

Gavana awarudisha kazini mawaziri kisha kuwapiga kalamu tena

October 2nd, 2018 1 min read

Na Kalume Kazungu

GAVANA wa Kaunti ya Lamu, Fahim Twaha aliwafuta kazi upya mawaziri wake wawili saa chache baada ya kuwarejesha kazini. Wawili hao, Bw Raphael Munyua Ndung’u (Afya na Mazingira) na Bi Florence Wairimu Ndung’u (Kilimo na Maji) walikuwa wamefutwa kazi miezi sita iliyopita lakini wakarudishwa kazini Alhamisi kufuatia amri ya mahakama.

Aidha kurejeshwa kwao kazini kulikuwa kwa muda tu kwani baadaye Bw Twaha aliwafuta kazi tena.

“Mawaziri hao awali walikuwa wamepigwa kalamu lakini walipoenda kortini, mahakama ilidai mpangilio uliotumika kuwafuta kazi haukufaa. Gavana alitii amri ya korti na akawarudisha mawaziri hao kazini. Sasa ameafikia kuwafuta kazi kwa kufuata mpangilio ufaao,” akasema mmoja wa maafisa wakuu wa serikali ya kaunti ya Lamu aliyeomba asitajwe.

Katika mahojiano na Taifa Leo Jumapili, Bw Ndung’u alithibitisha kupokea barua rasmi ya kuwafuta kazi.

Uamuzi wa mahakama kupitia kwa Jaji Linnet Ndolo uliotolewa Septemba 20, uliagiza serikali ya kaunti ya Lamu kuwarejesha kazini mara moja wawili hao hasa baada ya sababu zilizopelekea kufutwa kwao kukosekana.

Juhudi za kumpata Katibu wa Kaunti, Bw John Mburu Kimani ili kuzungumzia suala hilo ziligonga mwamba kwani simu yake ilikuwa imezimwa.