Habari

Gavana Awiti 'awapoteza' maseneta kwa kuwasilisha stakabadhi ya Kijerumani

November 15th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

GAVANA wa Homa Bay Cyprian Awiti aliwashangaza maseneta Alhamisi alipowasilisha mbele yao barua ambayo ilikuwa imeandikwa kwa lugha ya Kijerumani ikielezea sababu zilizosababisha yeye kukosa kufika mbele yao tangu mwaka 2018.

Kwa mara kadha, gavana huyo amekosa kufika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu wa Fedha za Umma (CPAIC) kujibu maswali kuhusu hitilafu katika usimamizi wa fedha katika serikali yake zilizoibuliwa katika ripoti za mkaguzi wa hesabu za serikali.

Alhamisi alijitetea akisema kuwa amekuwa akipokea matibabu katika mataifa ya Ujerumani na India baada ya kuugua maradhi ya macho.

Aliwashangaza wanachama wa kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang’ alipowasilisha stabadhi iliyoandikwa kwa Kijerumani ikielezea sababu zilizochangia kutofika kwake mbele yao.

“Sasa mbona umewasilisha barua hii iliyoandikwa kwa Kijerumani ilhali hii sio mojawapo ya lugha za matumizi katika bunge la Kenya? Si ungepeleka hati hii itafsiriwe kabla ya kuileta hapa?” akauliza Seneta wa Narok Ladema Ole Kina.

Hata hivyo, gavana huyo alijibu kwa kusema: “Nimewasilisha stakabadhi hii kwa sababu nilitaka mridhike kwamba kweli nilikuwa nchini Ujerumani kwa matibabu.”

Bw Awiti vilevile aliwataka maseneta hao kutomwadhibu kwa sababu hangeweza kusoma vizuri baadhi ya stakabadhi zenye taarifa kuhusu matumizi ya fedha katika kaunti yake kwa muda wote alipokuwa ng’ambo kwa matibabu.

Gavana wa Kaunti ya Homa Bay Cyprian Awiti alipofika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu wa Fedha za Umma (CPAIC) Novemba 14, 2019, kujibu maswali kuhusu hitilafu katika usimamizi wa fedha katika serikali yake zilizoibuliwa katika ripoti za mkaguzi wa hesabu za serikali. Picha/ Jeff Angote

“Nimekuwa mgonjwa. Hata wakati huu siwezi kusoma vizuri. Tangu mwanzoni mwa mwaka 2019 nimekwenda Ujerumani na India kwa matibabu. Macho yangu yananitatiza zaidi,” akasema Bw Awiti.

Awali kulikuwa na uvumi kwamba Bw Awiti alipoteza uwezo wa kuona baada ya kufanyiwa upasuaji katika hospitali moja jijini Nairobi mnamo Aprili 2019.

Ni baada ya hapo ambapo alielekea Ujerumani kwa matibabu.

Wakati ambapo Gavana Awiti hakuwepo ofisini, naibu wake Bw Hamilton Orata ndiye amekuwa akishika usukani.

Katika kikao cha Alhamisi kamati ya CPAIC iliitaka serikali ya Homa Bay kuwasilisha ripoti kuhusu mradi wa afya wa kiasi cha Sh3.8 bilioni uliokwama na hali katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Homa Bay.