Gavana hatarini kwa kumpa mkewe mamlaka ya kusimamia kaunti

Gavana hatarini kwa kumpa mkewe mamlaka ya kusimamia kaunti

Na Manase Otsialo

GAVANA wa Wajir Mohamed Abdi amejipata mashakani kwa mara ya pili katika muda wa miezi minane, baada ya madiwani wa kaunti hiyo kuwasilisha tena hoja ya kumtimua.

Wanadai Gavana Abdi amekiuka sheria na kutumia vibaya mamlaka ya ofisi yake miongoni mwa shutuma nyingine.Hoja hiyo mpya iliyotiwa saini na takriban madiwani 34 imefadhiliwa na Diwani wa Tulatula, Abdullahi Isack.

Inamshutumu Bw Abdi kwa ufisadi uliokithiri katika serikali yake, ukiukaji wa sheria na matumizi mabaya ya mamlaka.

Kulingana na nakala zilizowasilishwa katika Bunge la Wajir, Wawakilishi hao wa Wadi (MCAs) wanadai kwamba gavana alimwachia mkewe, Bi Kheira Omar, majukumu ya kuendesha kaunti.

Mnamo Agosti mwaka jana MCAs hao walisitisha mipango ya kumtimua Bw Abdi kufuatia upatanisho ulioendeshwa na viongozi kutoka Wajir kwa lengo la kubuni maafikiano kati ya serikali na Bunge la kaunti hiyo. Madiwani hao, hata hivyo, sasa wanamshutumu Gavana Abdi kwa kukiuka makubaliano waliyoafikiana.

“Tulitia saini mkataba wa maelewano lakini G-avana amekosa kutekeleza alichoahidi katika mkataba huo. Sasa hatuna hiari ila kumtimua aende nyumbani,” alisema Bw Isack.

Aliongeza: “Ni wazi kuwa Gavana Abdi hayuko usukani na badala yake ameachia mkewe majukumu anayostahili kutekeleza yeye mwenyewe.“Ugatuzi ulikuja kusuluhisha matatizo yaliyokuwa yamesonga Wakenya, lakini hapa Wajir watu wameongezewa mateso sababu gavana amepuuzilia mbali majukumu yake.”

 

You can share this post!

Mahangaiko tele familia zilizofurushwa katika ardhi zao...

CECIL ODONGO: Mbinu anazoweza kutumia Ruto ili kutwaa urais...