Habari

Gavana Joho alazwa akiugua Malaria

November 8th, 2019 1 min read

Na AMINA WAKO

GAVANA wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho amelazwa katika Hospitali ya Mombasa akiugua Malaria, amethibitisha Mkurugenzi wa Mawasiliano Richard Chacha.

Chacha ameambia Taifa Leo gavana huyo alipelekwa hospitalini Jumatano baada ya kuugua ghafla ambapo alikuwa na maumivu ya kichwa.

Madaktari walipendekeza alazwa hospitalini humo ili akaguliwe zaidi kitabibu.

Chacha hata hivyo ameelezea imani kwamba Joho ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama cha ODM anatarajiwa kuondolewa hospitalini Ijumaa.

Mapema Ijumaa aliyekuwa Rais wa Nigeria, Olusegun Obasanjo ambaye alitawala baina ya mwaka 1999 na 2007 amemtembelea hospitalini humo.

Gavana alionekana hadharani Oktoba 26, 2019, Malindi akiwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga katika mazishi ya Michael Ngumbao aliyefariki baada ya kupigwa risasi Oktober 15, 2019, siku mbili kuelekea uchaguzi mdogo wa kiti cha udiwani Ganda.