Habari MsetoSiasa

Gavana kikaangoni kutumia fedha zaidi kulipa mishahara

July 31st, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI ya kaunti ya Siaya inayoongozwa na Gavana Cornel Rasanga jana ilielekezewa lawama kwa kutumia pesa kuliko inavyohitajika kisheria, kugharimia ulipaji wa mishahara ya wafanyakazi huku miradi ya maendeleo ilitengewa mgao finyu.

Taarifa ya matumizi ya fedha ya kaunti hiyo katika mwaka wa kifedha wa 2017/2018 iliyowasilishwa mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (CPAIC) ilionyesha kuwa kaunti hiyo ilitumia asilimia 41 ya mapato yake kwa mishahara huku miradi ya maendeleo ikitengewa asilimia 17 pekee.

“Stakabadhi zilizoko mbele yetu zinaonyesha kuwa serikali ya Siaya ilitumia asilimia 41 ya mapato yake kulipia mishahara ya wafanyakazi, asilimia 12 ikatengewa Bunge la Kaunti na asilimia 30 ikatumika katika operesheni za kawaida. Hii ina maana kuwa ni asilimia 17 pekee zilitengewa miradi ya maendeleo badala ya asilimia 30 inavyohitajika kisheria,” akasema mwenyekiti wa kamati hiyo Moses Kajwang’.

Kulingana na sheria ya usimamizi wa fedha za umma (PFM Act) kaunti zinapasa kutumia asilimia 31 pekee ya mapato yao kugharimia mishahara ya wafanyakazi.

Gavana huyo alikabiliwa na wakati mgumu kutetea matumizi ya Sh351 milioni kulipia mishahara ya wafanyakazi katika mwaka huo wengi wao wakiwa nje ya orodha rasmi ya malipo ya wafanyakazi.

“Tunashuku kuwa huenda baadhi ya wafanyakazi hawa, haswa wale walioorodheshwa kama vibarua ni hewa kwa sababu wengi wana akaunti za benki nje ya kaunti ya Siaya. Orodha hii inaonyesha kuwa baadhi yao wamefungua akaunti katika matawi ya benki zilizoko katika miji ya Kisumu na Busia, ishara kwamba huenda ni wafanyakazi bandia,” akasema Seneta wa Kiambi Kimani Wa Matang’i.

Wanachama wa kamati ya CPAIC walilalamika kuwa licha ya kaunti ya Siaya kupokea Sh5.8 bilioni kama mgao kutoka hazina ya kitaifa na kukusanya Sh700 milioni kama ushuru na ada nyinginezo katika mwaka wa kifedha wa 2017/2018 haikutenga asilimia 30 ya fedha hizo kwa miradi ya maendeleo.

Seneta Fatuma Dullo (Isiolo) alihoji hatua ya serikali ya Gavana Rasanga kuajiri wafanyakazi wengi vibarua katika Idara za Mazingira na Usafi na ile ya Afya kuliko idara nyinginezo, akisema huenda hatua hiyo ilichukuliwa kimakusudi kutoa nafasi ya wizi wa fedha za umma.