Habari Mseto

Gavana Mutahi Kahiga asisitiza hang'atuki kutoka mrengo wa 'Team Ruto'

April 25th, 2019 1 min read

Na MWANGI MUIRURI

GAVANA wa Nyeri, Mutahi Kahiga amejitenga na habari kuwa amehama mrengo unaowekeza imani kisiasa na urais wa Dkt William Ruto katika uchaguzi wa 2022.

“Sitaki niingizwe katika mjadala wa kudhihaki wengine. Mimi sio kigeugeu katika maisha yangu. Mimi ni mzee ambaye anang’ang’ania
kubakia na ustaarabu hasa katika uamuzi. Mimi kwa sasa sitaki niorodhweshwe kwa wasiojielewa na nikakupa sababu,” Kahiga akaambia mtandao wa Taifa Leo.

Alisema kuwa hakuna siku hata moja alijitenga na wajibu wake wa kumwamkua Dkt Ruto akiwa katika ziara Kaunti ya Nyeri.

“Nitakwepa kumlaki Dkt Ruto kwa msingi gani ilihali yeye ndiye Naibu Rais? Ikiwa mimi kama kiongozi nitakuwa katika siasa za kubishana
na afisi ya kikatiba hapa nchini na ambayo ni matokeo ya kura ya wananchi ambao pia mimi wamenichagua, nitakuwa nacheza siasa gani?”
akahoji.

Bw Kahiga ambaye ni gavana wa nne katika Kaunti hiyo ambapo wa kwanza alikuwa Nderitu Gachagua aliyeaga dunia akiwa anahudumia awamu yake ya kwanza na kikatiba Naibu wake, Samuel Wamathai akawajibishwa usukani.

Katika uchaguzi mkuu wa 2017, Wahome Gakuru alichaguliwa kuwa Gavana, lakini akaishia kuaga dunia kabla ya kuhudumu kwa mwaka mmoja na ndipo Kahiga akiwa naibu aliwajibishwa usukani.

Katika msingi huo, Bw Kahiga alisema kuwa Kaunti yake imekuwa ikikumbana na changamoto nyingi na “kwa sasa siwezi kuwa na wakati wa
kujiingiza katika siasa za kuhujumu afisi ya Naibu Rais.”

Alisema kuwa afisi hiyo ya Naibu Rais inafaa kuheshimiwa na wote “sio kwa msingi kuwa ni Dkt Ruto ambaye kwa sasa amekalia kiti cha
afisi hiyo bali kwa kuwa ni afisi ya kikatiba na ambapo kwa muda mwingi ujao, kiti hicho kitakuwa na anayekikalia.”

Alisema kuwa siasa za kuhujumiana ndizo zimenoga katika ulingo wa siasa kwa sasa, akisema kuwa hali hiyo haifai kwa kuwa haizidishii
Wakenya huduma za kimaendeleo.