Habari Mseto

Gavana Mutua na Keter roho mkononi wakisubiri hatima Ijumaa

December 19th, 2018 1 min read

Na BENSON MATHEKA

GAVANA wa Kaunti ya Machakos, Dkt Alfred Mutua na mbunge wa Nandi Hills Alfred Keter, mnamo Ijumaa watajua iwapo wataendelea kuhudumu au watarudi kwenye debe, Mahakama ya Juu itakapotoa uamuzi kuhusu kesi zao za uchaguzi.

Naibu Msajili wa Mahakama hiyo Daniel Ole Keiwua alisema kesi za Dkt Mutua na Bw Keter ni miongoni mwa 13 zitakazoamuliwa Ijumaa.

Dkt Mutua aliwasilisha rufaa katika Mahakama ya Juu baada ya uchaguzi wake kubatilishwa na Mahakama ya Rufaa ambayo ilipata kuwa hakushinda kwa njia huru na ya haki. Mgombeaji wa chama cha Wiper Wavinya Ndeti alikata rufaa baada ya kukosa kuridhishwa na uamuzi wa Jaji Aggrey Muchelule wa Mahakama Kuu kwamba Dkt Mutua wa chama cha Maendeleo Chap Chap alikuwa ameshinda uchaguzi wa Agosti 17 2017 kwa haki.

Ushindi wa Bw Keter ulioidhinishwa na Mahakama ya Rufaa unapingwa na Bw Benard Kitur ambaye alikimbia katika Mahakama ya Juu akilalama kwamba majaji Erastus Githinji, Fatuma Sichale na Hannah Okwengu walikosea kwa kubatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu iliyokuwa imebatilisha ushindi wa mbunge huyo mbishani wa chama cha Jubilee.

Gavana mwingine ambaye atajua hatima yake Ijumaa ni Salim Mvurya wa Kwale wa chama cha Jubilee ambaye ushindi wake unapingwa na wapigakura watatu wa kaunti hiyo.

Mbunge wa Embakasi Kusini Julius Mawathe pia atajua hatima yake siku hiyo katika kesi anayopinga kubatilishwa kwa ushindi wake.

Kesi ya kupinga ushindi wake iliwasilishwa na Ishrad Sumra wa chama cha ODM.

Mahakama pia itaamua kesi za uchaguzi za maeneobunge ya Kilgoris, Ugenya, Bonchari na kiti cha mwakilishi wa wanawake kaunti ya Masarbit.