Siasa

Gavana Nanok abanwa kwa kutotumia Sh3.7b za kaunti

September 3rd, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MASENETA wamempa Gavana wa Turkana Josephat Nanok wiki mbili aeleze sababu za serikali yake kutotumia Sh3.7 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2017/2018 na kuwakosesha wakazi thamani ya fedha hizo.

Wanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu wa Fedha za Umma (CPAIC), inayoongozwa na Seneta wa Kisii Sam Ongeri, walimwambia Bw Nanok kuwa hakuna haja kwa kaunti yake kudai nyongeza ya mgao wa fedha kutoka hazina ya kitaifa ikiwa haiwezi kutumia kikamilifu fedha inazotengewa.

‘Hali kama hii inamvunja moyo Seneta wa Turkana Profesa Malachy Ekal ambaye wakati huu yuko mstari wa mbele kupigania kaunti hii isipunguziwe pesa chini ya mfumo wa ugavi wa fedha ulioleta utata,’ akasema Prof Ongeri.

“Kwa hivyo, baada siku 14 tunataka maelezo kamili kutoka kwake la sivyo makosa haya yatakuandama hadi utakapoondoka afisini mnamo 2022,” akaongeza.

Bw Nanok alikuwa amefika mbele ya kamati hiyo Jumanne kujibu maswali kuhusu hitilafu katika matumizi ya fedha yaliyoibuliwa kwenye ripoti ya aliyekuwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Edward Ouko katika mwaka huo wa kifedha wa 2017/2018.

Naye Seneta wa Nandi Samson Cherargei alisema Sh3.7 bilioni ambazo kaunti ya Turkana ilikosa kutumia katika mwaka huo wa kifedha ni sawa na asilimia 90 ya mgao wa fedha kwa kaunti jirani ya Elgeyo Marakwet, iliyopokea Sh4.5 bilioni kutoka hazina kuu mwaka huo wa kifedha.

‘Ikiwa kaunti ya Turkana haina uwezo wa kutumia kiasi hiki cha fedha hiyo ni sababu tosha kwamba inapasa kupunguziwa mgao wa fedha na badala yake kaunti kama vile Elgeyo Marakwet, Nandi au Pokot Magharibi ziongezewe fedha hizo. Ni makosa kwa kaunti ya Turkana kukosa kutumia fedha ilhali wengi wa wakazi wake ni maskini,’ akaongeza Bw Cherargei.

Lakini akijitetea, Gavana Nanok alitaja sababu kadha zilizopelekea kaunti yake kukosa kutumia kiasi hicho cha fedha, ikiwemo Hazina ya Kitaifa kutuma pesa kuchelewa.

‘Vile vile kaunti yangu haina wataalamu na wahandishi hitajika wa kufanikisha utekelezaji wa miradi na mipango ikizingatiwa kuwa wengi wao hawataki kufanya kazi katika kaunti ya Turkana ambayo ni kame. Ukosefu wa wataalamu hawa umechelewesha utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo,’ akasema Nanok.

Kiranja wa wengi Irungu Kang’ata na Seneta wa Migori Ochilo Ayacko walisema ni kinaya kwamba kaunti ya Turkana haina wataalamu wa kufanya kazi katika idara mbalimbali ilhali Kenya inakabiliwa na uhaba mkubwa wa ajira.

‘Ningetaka Gavana Nanok atoe ushahidi kuonyesha kuwa serikali yake ilitangaza nafasi za kazi lakini watalaamu waliohitajika hawakuwasilisha maombi. Ikiwa hali ni hiyo katika kaunti ya Turkana basi naalika Gavana Nanok aje Murang’a nimpe wafanyakazi katika taaluma zote,’ akasema Bw Kang’ata ambaye ni Seneta wa Murang’a.

Bw Nanok alieleza kuwa kaunti yake ina msanifu majengo (Architect) mmoja pekee huku alisimilia 80 ya wahudmu wa afya sio wenyeji.

‘Hali kama hiyo inaathiri sekta ya elimu ambapo tunategemea pakubwa watu kutoka kuanti zingine,’ akasema.

Lakini Bw Ayacko alimshauri Gavana Nanok kutenga hazina maalum ya kufadhili mpango wa kutoa udhamini wa masomo kwa wenye wa Turkana katika taaluma mbalimbali.

‘Serikali ya Turkana inafaa kuwekeza kwingi katika mpango wa kutoa mafunzo ya kitaalum kwa wenye wa kaunti hiyo ili baada ya miaka michache iweze kupata nguvu kazi hitaji kusukuma gurudumu la maendeleo,’ akasema Bw Ayacko.