Habari za Kaunti

Gavana Nassir apambana kuepuka kutupwa Shimo La Tewa

May 17th, 2024 2 min read

NA PHILIP MUYANGA

GAVANA wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir na maafisa wawili wakuu wa kaunti hiyo wameomba mahakama iondoe maagizo yaliyotolewa kuwa wakamatwe na kufungwa jela ya Shimo la Tewa miezi mitatu kwa kukaidi korti.

Kupitia wakili Murtaza Tajbhai, Bw Nassir, Waziri wa Ardhi wa Kaunti Mohamed Hussein na Mwanasheria Mkuu wa Kaunti Jimmy Waliaula wanasema kuwa walihukumiwa bila kusikilizwa wala kutendewa haki.

Bw Nassir na maafisa hao wawili wanasema hakuna agizo lolote la mahakama ambalo walipewa na kwamba uhuru wao uko hatarini.

“Athari za maagizo hayo ya Machi 13 na Aprili 24 kutoka kwa mahakama hii ni yale ya kuchukua uhuru wa watu na kiwango kiangaliwacho sio uwezekano tu lakini zaidi ya ushahidi,” alisema wakili Tajbhai katika ombi lake.

Kampuni ya Innovative Properties Ltd ilitaka Bw Nassir na maafisa hao wawili wa kaunti kupatikana na hatia ya kukiuka agizo la mahakama, mojawapo likiwa ni agizo la kudumu la kuwazuia washtakiwa, mawakala wao au mtu yeyote kuwepo, kuingia bila ruhusa au kutwaa kipande cha ardhi kilicho katika barabara ya Abdel Nasser, Mombasa.

Nassir, Hussein na Waliaula walidai kuwa hali iliyojitokeza kwa mahakama ni kwamba walikiuka maagizo ya mahakama na wanaendelea kufanya hivyo, ambapo si hivyo, kwani wanaheshimu mamlaka ya mahakama.

Machi 13, 2024, mahakama ilikuwa imetoa agizo la kuwa watatu hao wafike mahakamani kuelezea kwa nini wasifungwe jela kwa miezi sita kwa kutotii agizo la mahakama lililotolewa Januari mwaka wa 2021.

Mnamo Aprili 24, mahakama ilitoa agizo la kukamatwa kwa Bw Nassir, Hussein na Waliaula baada ya kuwahukumu kifungo cha miezi mitatu katika gereza la Shimo la Tewa kuanzia Mei 10, kwa kukiuka agizo la mahakama.

Hata hivyo,mahakama ilisimamisha kwa muda utekelezaji wa agizo hilo kabla ya kusikizwa na kuamuliwa kwa ombi lao la kutaka maagizo ya kuwapata na hatia ya kukiuka agizo la mahakama kufutiliwa mbali.

Kupitia wakili Willis Oluga, Innovative Properties Ltd inasema kuwa Nassir,Hussein na Waliaula ni maafisa wakuu wa serikali ya Kaunti ya Mombasa na mahakama inafaa kuchukua hatua kali dhidi yao ili wawe kielelezo kwa maafisa wengine kuhusiana na athari za kukiuka agizo la mahakama.

Bw Oluga anayetaka ombi la watatu hao kutupiliwa mbali alisema madai ya kuwa maafisa hao wa kaunti wanaheshimu mamlaka ya mahakama sio ukweli.

“Hawajaonyesha juhudi zozote, wamefanya kutatua suala la kuingiliwa bila ruhusa kwa kipande cha ardhi kinyume na agizo la mahakama,” alisema Bw Oluga.

Alisema maafisa hao wa kaunti hawajafika mahakamani kwa ‘roho safi’ kwani mbali na kudanganya katika kiapo, hawajatatua suala la kuendelea kwao kukiuka agizo la korti ambapo wamewaacha wafanyakazi wao kuendelea kukaa katika ardhi hiyo.

Katika ombi lao, kampuni hiyo ilisema washtakiwa walikataa makusudi kufuatilia uamuzi wa Jaji CK Yano licha ya kukumbushwa kufanya hivyo.

Kulingana na kampuni hiyo, maafisa wa serikali ya Mombasa wamekiuka na wanaendelea kukiuka uamuzi wa mahakama kwa kuwaruhusu wafanyakazi wao kuendelea kukaa na kutumia ardhi hiyo huku wakihitilafiana na utumizi dhidi ya maagizo yaliyotolewa.

Kesi itatajwa Julai 8, 2024.