Habari za Kaunti

Gavana Nassir na maafisa wake wawili hatarini kufungwa

April 27th, 2024 1 min read

NA BRIAN OCHARO

GAVANA wa Mombasa Abdulswamad Nassir, Wakili wa Kaunti Jimmy Waliaula na Afisa Mkuu Mtendaji wa Ardhi Mohammed Hussein Mohamed, watafungwa jela iwapo mazungumzo na kampuni ya kibinafsi kuhusu ardhi ya mabilioni ya pesa hayatazaa matunda.

Mahakama ya Mazingira na Ardhi imewapa muda watatu hao kujadiliana na wasimamizi wa kampuni ya Innovate Property Limited kutatua mzozo wa kudharau amri ya mahakama kuhusu ardhi hiyo ya mabilioni ya pesa.

Jaji Lucas Naikuni ameongeza hadi Mei 6, 2024, agizo la kuwataka watatu hao kueleza kwa nini hawapaswi kufungwa jela kwa kudharau amri ya mahakama ili kuruhusu mazungumzo hayo muda wa kutosha.

“Wakati huo huo, ninaendelea kuwahukumu watatu hao kutumikia kifungo cha miezi mitatu jela ya kiraia katika gereza la Shimo La Tewa kuanzia Mei 10, 2024, kwa kudharau amri ya mahakama,” alisema jaji huyo.

Jaji Naikuni mnamo Machi 7, 2024, alimtaka Bw Nassir kufika mbele ya mahakama yake ili kuelezea ni kwa nini hapaswi kufungwa jela kwa kushindwa kuwaondoa maafisa wake kutoka kwa ardhi yenye ukubwa wa hekta 0.2641 iliyo kando ya Barabara ya Abdel Nassir mjini Mombasa, inayomilikiwa na kampuni ya Innovative Properties Limited.

Kampuni hiyo inahoji kuwa mahakama ilikuwa imetoa maagizo miongoni mwao ya kubatilisha hati kuhusu ardhi hiyo.

Agizo jingine, kampuni hiyo inasema lilikuwa ni zuio la kudumu la kuwazuia washtakiwa, mawakala wao au mtu yeyote kuingilia au kumiliki ardhi hiyo.

Kupitia wakili Willis Oluga, kampuni hiyo ilisema kuwa washtakiwa walikataa kimakusudi kuheshimu uamuzi wa mahakama licha ya kukumbushwa mara kwa mara.