Habari Mseto

Gavana Nyagarama afariki baada ya kuugua

December 18th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

GAVANA wa Kaunti ya Nyamira John Obiero Nyagarama amefariki katika Nairobi Hospital kufuatia kile kinachotajwa ni matatizo ya kiafya yaliyochangiwa na Covid-19.

Amekuwa na umri wa miaka 74.

Mwanawe wa kiume, Momanyi Nyagarama amethibitisha Ijumaa kifo cha babake ambaye alikuwa akihudumu kipindi cha pili na cha mwisho.

Katika siku za hivi karibuni uvumi umekuwa ukizagaa kuhusu hali ya afya yake Gavana Nyagarama haswa baada ya kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika Nairobi Hospital majuma mawili yaliyopita.

Hata hivyo, maafisa wa serikali ya Kaunti ya Nyamira na watu wa familia yake hawakufichua ugonjwa ambao ulikuwa ukimzonga kiongozi huyo.

Hata hivyo, Gavana Nyagarama alipatikana na matatizo ya kiafya miaka miwili iliyopita na kusababisha kulazwa kwake katika hospitali moja nchini Amerika kwa miezi miwili akipokea matibabu.

Mwanasiasa huyo zamani alifanya kazi kama mwalimu wa shule ya sekondari kabla ya kupiga mbizi katika siasa alipowania ugavana wa Nyamira 2013 kwa tiketi ya ODM na kushinda.

Alitetea kiti hicho katika uchaguzi mkuu wa 2017 na kuweza kudumisha ushindi wake, akipeperusha bendera ya ODM licha ya kuwepo kwa mawimbi makali ya chama cha Jubilee katika kaunti hiyo.

Marehemu Nyagarama alisomea katika shule ya msingi ya Nyakemincha iliyoko eneobunge la Mugirango Magharibi kisha akajiunga na shule ya upili ya Maseno alikosomea hadi Kidato cha Nne.

Baadaye alijiunga na shule ya upili ya Kisii School katika kidato cha tano na sita kabla ya kijunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kusomea ualimu wa masomo ya Lugha ya Kiingereza na Fasihi. Alihitimu kwa shahada ya ualimu mnamo 1975.